Jengo la Kiambu laanza kuzama, wapangaji wahimizwa kuondoka

Zaidi ya wapangaji 20 katika jengo moja kaunti ya Kiambu, eneo la Kiamumbi wamehimizwa kuondoka.

Muhtasari

•Gavana wa Kiambu Kimani Wamatangi alisema kuwa serikali ya kaunti itafanya kila iwezalo kuwasaidia walioathiriwa.

•Wamatangi alisema kuwa serikali ya kaunti inafanya kila iwezalo kuwasaidia wale walio katika hali mbaya

Wakazi waondoka kwenye jumba linalosemekana kuwa karibu kuzama Mei 2, 2024.
Wakazi waondoka kwenye jumba linalosemekana kuwa karibu kuzama Mei 2, 2024.
Image: AMOS MBURU

Zaidi ya wapangaji 20 katika jengo moja kaunti ya Kiambu, eneo la Kiamumbi wamehimizwa kuondoka.

Ghorofa ilianza kutengeneza nyufa na baadaye ikaanza kuzama.

Akizungumza wakati wa ukaguzi, gavana wa Kiambu Kimani Wamatangi alisema kuwa serikali ya kaunti itafanya kila iwezalo kuwasaidia walioathiriwa.

Aliwaagiza maafisa wa polisi na wenyeji kukesha na kuruhusu wapangaji wote kuondoka.

"Ningependa kuwasihi wenyeji na wapangaji kukwepa jengo hili. Si salama kwa makazi," Wamatangi alisema.

Aidha alisema kuwa serikali ya kaunti inafanya kila iwezalo kuwasaidia wale walio katika hali mbaya

“Serikali ya kaunti iko tayari kuwasaidia walioathiriwa na mvua inayoendelea kunyesha na tumeazimia kutatua suala lolote,” akasema.

MCA wa mtaa wa Kiambu Francis Koina alisema kuwa walioathiriwa wanaweza kutafuta hifadhi katika kanisa la ACK Kiamumbi.

"Wale walioathiriwa wanaweza kutafuta hifadhi katika kanisa la ACK na kutoka hapo tunaweza kutoa usaidizi wowote kutoka kwa serikali ya Kaunti," alisema.