Kenya yatuma vifaa vya uokoaji na boti katika maeneo yaliyokumbwa na mafuriko

Operesheni za anga na majini zinaendelea kuokoa makumi ya familia zilizokwama katika makazi yao.

Muhtasari

•Siku ya Jumamosi, Mto Nyando ulipasua kingo zake, na kuzamisha vijiji kadhaa na kulemaza usafiri kwenye barabara kuu ya Kisumu-Nairobi.

•Zaidi ya kaya 1,000 zililazimika kukimbia makazi yao, vyombo vya habari vya ndani viliripoti.

Image: BBC

Operesheni za anga na majini zinaendelea kuokoa makumi ya familia zilizokwama katika makazi yao katika eneo la Nyando Magharibi mwa Kenya huku kukiwa na mafuriko yanayoendelea kote nchini.

Siku ya Jumamosi, Mto Nyando ulipasua kingo zake, na kuzamisha vijiji kadhaa na kulemaza usafiri kwenye barabara kuu ya Kisumu-Nairobi.

Zaidi ya kaya 1,000 zililazimika kukimbia makazi yao, vyombo vya habari vya ndani viliripoti.

Hakukuwa na ripoti za mara moja za majeruhi lakini polisi wa eneo hilo walisema viwango vya maji bado vinaongezeka.

Timu ya pamoja ya Shirika la Msalaba Mwekundu la Kenya, Huduma za Walinzi wa Pwani ya Kenya na Huduma ya Wanyamapori ya Kenya (KWS) wanatumia boti na helikopta kufikia vijiji vilivyofunikwa na maji.

Helkopta ya Shirika la Kenya Wildlife Services (KWS) inawasafirisha kwa ndege waliookolewa, huku kukiwa na hofu kwamba familia nyingi zililala kwenye baridi katika vijiji vilivyoathiriwa.

Haya yanajiri huku serikali ikiwahamisha watu zaidi kutoka maeneo yanayokumbwa na mafuriko.

Rais William Ruto Jumatatu alisema serikali itaipa kila familia iliyoathiriwa $70 (£60) ili kuwasaidia kutafuta makazi mbadala kwa miezi mitatu.

Katika taifa zima, mafuriko hayo yamegharimu maisha ya watu 228 tangu Machi, huku 72 wakiwa bado hawajulikanu walipo, kulingana na takwimu za serikali.

Kenya na nchi jirani ya Tanzania ziliepuka uharibifu mkubwa wa Kimbunga Hidaya kilichopungua baada ya kupiga Jumamosi.