Shule zote kufunguliwa Jumatatu, Mei 13- Rais Ruto atangaza

Rais William Ruto ametangaza kuwa shule zote zitafunguliwa Jumatatu, Mei 13.

Muhtasari

•Tangazo hili linakuja wiki moja tu baada ya serikali kusimamisha shughuli ya kufunguliwa tena kwa shule.

Rais William Ruto
Rais William Ruto
Image: PCS

Rais William Ruto ametangaza kuwa shule zote zitafunguliwa Jumatatu, Mei 13.

Tangazo hili linajiri wiki moja tu baada ya serikali kuahirisha kwa mara ya pili ufunguzi wa shule hadi ilani nyingine kutolewa.

Rais alitoa tangazo hilo wakati wa mkutano na viongozi kutoka kaunti za Laikipia na Kajiado katika Ikulu ya Nairobi.

Akizungumza wakati wa mkutano huo, Rais Ruto alieleza kuwa shule zitafunguliwa wiki ijayo, baada ya kupokea ripoti kutoka kwa idara ya utabiri wa hali ya hewa  ya Kenya, iliyoashiria kuwa kiwango cha mvua kimepungua katika maeneo mbali mbali nchini.

Hii ilikuwa baada ya serikali kuahirisha kufungua tena shule kwa muhula wa pili kutokana na mvua kubwa iliyosababisha mafuriko katika maeneo mbali mbali nchini.

Wakati huo huo, Rais Ruto ameagiza kuwa pesa za ujenzi wa miundomsingi ya shule zilizoharibiwa na mvua kubwa zipatikane kupitia Hazina ya Kitaifa ya Kustawisha Maeneo bunge ya Serikali (NG-CDF).

Awali ilikuwa imepangwa kuwa shule zingefunguliwa Aprili 29, 2024, lakini tarehe hiyo ilisogeshwa hadi Mei 6, 2024, kwa sababu ya mvua kubwa iliyokuwa ikinyesha nchini.

Rais Ruto Ijumaa wiki jana alikuwa ameagiza Wizara ya Elimu kuahirisha kufunguliwa kwa shule zote kwa muda usiojulikana kwa saobabau ya changamoto za mafuriko.