Ruto kununua sare za shule kwa wanafunzi katika shule ya msingi ya Lenana

Rais alisema hadi sasa serikali yake imejenga madarasa 22 na wanafunzi wasiopungua 1300 tayari wamejiunga na shule hiyo.

Muhtasari
  • Akizungumza wakati wa hafla hiyo, Ruto alisema taasisi hiyo ni ahadi aliyotoa miaka minne iliyopita wakati Shule ya Precious Talent ilipoporomoka.
Ruto kununua sare za shule kwa wanafunzi katika shule ya msingi ya Lenana
Image: RAIS WILLIAM RUTO/ X

Rais William Ruto Jumatatu alifungua rasmi shule ya msingi ya Lenana, ili kuhudumia wanafunzi karibu na eneo la Ng'ando eneo bunge la Dagoretti Kusini.

Akizungumza wakati wa hafla hiyo, Ruto alisema taasisi hiyo ni ahadi aliyotoa miaka minne iliyopita wakati Shule ya Precious Talent ilipoporomoka.

"Shule hii ilijengwa na serikali kusaidia watoto kuzunguka eneo hili. Nilikuwa hapa miaka minne iliyopita tulipopoteza wanafunzi wetu katika mkasa wa shule ya kibinafsi. Sasa ninatimiza ahadi niliyotoa wakati huo," Ruto alisema.

Rais alisema hadi sasa serikali yake imejenga madarasa 22 na wanafunzi wasiopungua 1300 tayari wamejiunga na shule hiyo.

Alisema vyumba hivyo vitachukua wanafunzi wa darasa la 1 hadi la 4, na kuna mpango wa kujenga vyumba vingine 24 ili kupisha madaraja mengine.

"Mimi binafsi nitahakikisha najenga madarasa 24 yaliyosalia na pia kuwanunulia madawati na madarasa mengine tisa ambayo naelewa hayana madawati. Pamoja na mbunge wa eneo lako (John Kiarie) tumejipanga kuhakikisha shule hii inawafaa. imekamilika," Ruto aliongeza.

Pia aliwasisimua wazazi na wanafunzi alipotangaza kuwa atamnunulia kila mwanafunzi sare kamili ya shule, vikiwemo viatu.

"Ninataka uongozi wa shule utafute watengeneza sare waje hapa na kuchukua vipimo kwa kila mwanafunzi anayefika katika shule hii. Nitamlipia kila mwanafunzi sare yake," Ruto alitangaza.