Wacheni kujadili mswada wa fedha matangani, Wetangula awambia wabunge

"Nyinyi ndio watu mnaokuja na mapendekezo ya bajeti kupitia kamati zenu, tafadhali okoa mateso ya umma"

Muhtasari

• Wetangula aliwataka wabunge kutumia mapumziko ya mwezi mmoja kutafakari Muswada wa kifedha.

• Spika wa bunge alisema kwamba ni kamati za bunge ndizo zilizotoa mswada huo wa bajeti hiyo.

SPIKA MOSES WETANGULA
Image: HISANI

Spika wa Bunge la Kitaifa Moses Wetang’ula amewasihi Wabunge hasa kutoka kwa upinzani kujiepusha na kukosoa Mswada wa Fedha wa 2024 unaopendekezwa katika mazishi na hafla zingine za umma na kusaidia umma kuuelewa vyema.

Kiongozi huyo wa Ford Kenya alizungumza katika eneo bunge la Kabuchai kaunti ya Bungoma siku ya Jumatano wakati wa mazishi ya Mzee Yonah Namuli.

Spika, hata hivyo, aliwataka wabunge kutumia mapumziko ya mwezi mmoja kutafakari Muswada huo wa kifedha akisema kwamba ni kamati za bunge ndizo zilizotoa bajeti hiyo.

"Nyinyi ndio watu mnaokuja na mapendekezo ya bajeti kupitia kamati zenu, tafadhali okoa mateso ya umma na mjiepushe kusimama mbele ya umma na kulalamika sana kuhusu Muswada wa Fedha wa 2024 na ilhali ni nyinyi ndio mnapaswa kutoa mapendekezo ya bajeti," Wetang'ula alisema.

"Wabunge wanapaswa kuketi na kufanya mambo ambayo yanaweza kuwanufaisha watu wa Kenya, wapiga kura wanawategemea na wanawaamini kwa sababu waliwapigia kura."

Wetang’ula aliwaomba wakazi wa Bungoma kuunga mkono serikali ya Rais William Ruto inayoangazia miradi ya maendeleo inayoendelea katika kaunti hiyo.

Wetang’ula alitoa mfano wa ujenzi unaoendelea wa masoko ya Chwele, Chebukube na Kamukunywa unaogharimu Shilingi milioni 300 huko Kimilili.

Pia aliangazia ukarabati wa barabara ya Malala-Kanduyi ambayo alisema itapandishwa hadhi na kuwa ya kiwango cha A ili kukidhi malori makubwa ya kibiashara.

Pia alisema kuwa serikali itatoa Shilingi milioni 25 kwa ajili ya upanuzi na ujenzi wa Chuo cha Mafunzo ya Matibabu cha Kenya (KMTC) katika eneo bunge la Kabuchai.

IMETAFSIRIWA NA DAVIS OJIAMBO.