Achana na siasa za Mlima Kenya! - Gachagua awazomea viongozi wa Bonde la Ufa

Gachagua alisema viongozi wa Bonde la Ufa wanapaswa kuzingatia siasa za eneo lao.

Muhtasari

•Gachagua amewataka viongozi wa Bonde la Ufa kuachana na siasa za Mlima Kenya akisema ni ngumu sana kwao kuzishughulikia.

akitangamana na wanawake wakati wa mpango wao wa kuwawezesha katika Kesses, kaunti ya Uasin Gishu Jumamosi, Mei 25, 2024.
Naibu Rais Rigathi Gachagua akitangamana na wanawake wakati wa mpango wao wa kuwawezesha katika Kesses, kaunti ya Uasin Gishu Jumamosi, Mei 25, 2024.
Image: DPPS

Naibu Rais Rigathi Gachagua amewataka viongozi wa Bonde la Ufa kuachana na siasa za Mlima Kenya akisema ni ngumu sana kwao kuzishughulikia.

Naibu rais ambaye alikuwa akizungumza wakati wa kuchangisha fedha kwa ajili ya mpango wa kuwawezesha wanawake katika eneo la Kesses, Uasin Gishu, alishutumu baadhi ya viongozi kwa kupanga njama kubainisha ni viongozi wagani wafuatao katika Mlima Kenya.

Lakini katika onyo la wazi kwa viongozi hao, Naibu Rais alisema jitihada zao ni ubatili kwani siasa za Mlima Kenya ni ngumu zaidi kuliko wanavyofikiri.

"Mimi naomba watu wa bonde la ufa, tafadhali, sisi tuliunga Rais kwa hiari yetu na kwa kupenda na tunaendelea kumuunga mkono. Tunaomba heshima kidogo, msijaribu kutupangia siasa ya Mlima Kenya na kuptupangia uongozi," Gachagua alisema.

Gachagua alisema viongozi wa Bonde la Ufa wanapaswa kuzingatia siasa za eneo lao badala ya Mlima Kenya na kuongeza kuwa kamwe hawatafikiria kuchagua viongozi wa eneo hilo.

Naibu Rais aliwataka viongozi wa Bonde la Ufa kuangazia kumsaidia Rais William Ruto kutimiza ahadi zake za kampeni akisema kuendelea kuhusika katika siasa kutamfanya kushindwa.

Alikashifu kundi la viongozi kutoka eneo hilo na Mlima Kenya kwa kupanga njama za kumrithi Rais badala ya kulenga kumsaidia kufanikisha.

“Kumchagua kiongozi ni jambo moja na kufanikiwa ni sehemu ngumu, mimi nikiwa msaidizi mkuu wa Rais, jukumu langu ni kuhakikisha anafanikiwa, hilo ndilo lengo langu kwa sasa,” alisema.