Ghadhabu baada ya marufuku ya muguka Mombasa na Kilifi

Baadhi ya wafanyibiashara na wakulima wa muguka wamelalamika vikali kufuatia marufuku ya mmea huo .

Muhtasari

•Gavana wa Kilifi Gideon Mung’aro pamoja na gavana wa Mombasa Abdullswamad Sherrif Nassir waliamuru kufungwa kwa biashara ya uuzaji wa Muguka

•Viongozi wa Embu wametishia kuzipeleka mahakamani kaunti ya Mombasa na Kilifi  iwapo watazidi kupiga marufuku.

Miraa
Image: maktaba

Hali ya mshikemshike imetanda miongoni mwa wafanyibiashara na wakulima wanaokuza mmea almaarufu muguka.

Wengi wameghadhabishwa kutokana na marufuku ya mmea huo hasa kwenye magatuzi ya Mombasa na Kilifi wakisema kuwa wanategemea mmea huo kujipa riziki na kukimu mahitaji ya familia zao.

‘’Kama kuna biashara zao zimekuwa chini waseme ukweli waache kudanganya sababu hapa wananyima watu wengi haki,’’ ndivyo alivyosema mfanyibiashara mmoja wa Mombasa akizungumza na Citizen TV.

Gavana wa Kilifi Gideon Mung’aro pamoja na mwenzake wa Mombasa Abdullswamad Sherrif Nassir waliamuru kufungwa kwa biashara ya uuzaji wa Muguka katika kaunti zao kwani walisisitiza kuwa vijana wengi wamejitoma katika lindi la uraibu wa mihadarati na ya kwamba matumizi ya muguka yanaweza leta matatizo ya kiakili miongoni mwa vijana na kuwafanya kuwa punguani hasa ikizingatiwa kuwa vijana wenye umri wa makamu ndio waraibu zaidi.

Baadhi ya wakulima wa Embu waligadhabishwa na uamuzi huo na kusema ya kwamba kupigwa marufuku biashara ya muguka kunaweza athiri uchumi wa nchi kwani vijana wengi wanategemea ukulima huo kujistawisha na kujinufaisha kikazi. 

Mwakilishi wa kike Embu, Njoki Njeru, alikuwa na haya ya kusema, ''Wiki iliyopita tumepeana 126 million ile ambayo itagharamia mogoka na miraa, wakulima wa Embu na kule Meru kwa hivyo kama iyo pesa si halali basi serikali haingepeana.''

Viongozi wa Embu wametishia kuzipeleka mahakamani kaunti ya Mombasa na Kilifi  iwapo watazidi kupiga marufuku.

Je, kupigwa kwa marufuku kwa miraa kuna manufaa yapi hasa ukiwa umeorodheshwa kama mazao ya fedha almaarufu cash crop na serikali kuu? Fauka ya hayo, miraa ni kitega uchumi kwa wakulima wa mlima Kenya na umeidhinishwa na serikali kuu kwani ni nguzo mojawapo ya ukuaji wa uchumi na pia uti wa mgongo wa uchumi katika eneo la mlima Kenya.