Kenya yapokea ushahidi 'wa kuhuzunisha' dhidi ya wanajeshi wa Uingereza

"Ninachotaka tu ada ya matunzo ili mtoto wangu aweze kwenda shule na kuwa na maisha bora ya baadaye," alisema.

Muhtasari
  • Makumi ya watu wiki hii wametoa ushahidi mbele ya kamati ya bunge kuhusu madai ya utovu wa nidhamu wa wanajeshi kutoka Kitengo cha Mafunzo ya Jeshi la Uingereza Kenya (Batuk).

Jopo la uchunguzi wa kihistoria kuhusu madai ya ukiukaji wa haki za binadamu uliyofanywa na wanajeshi wa Uingereza nchini Kenya limekuwa likipokea ushahidi "wa kuhuzunisha" kutoka kwa wale wanaosema walidhulumiwa.

Makumi ya watu wiki hii wametoa ushahidi mbele ya kamati ya bunge kuhusu madai ya utovu wa nidhamu wa wanajeshi kutoka Kitengo cha Mafunzo ya Jeshi la Uingereza Kenya (Batuk).

Miongoni mwao ni familia ya msichana anayedaiwa kulemaa baada ya kugongwa na na lori la Jeshi la Uingereza, mama ambaye anasema alitelekezwa akiwa mjamzito na mwanamume aliyevamiwa na simba kufuatia moto unaodaiwa kuwashwa wakati wa zoezi la mafunzo ya kijeshi.

Kituo cha Batuk kilichopo Nanyuki, takriban kilomita 200 kaskazini mwa mji mkuu, Nairobi, na kilianzishwa mwaka wa 1964 muda mfupi baada ya taifa hilo la Afrika Mashariki kupata uhuru kutoka kwa Uingereza.

Waziri wa Ulinzi wa Kenya Aden Duale amesema kuwa Kenya itashinikiza mashtaka dhidi ya mwanajeshi yeyote wa Uingereza anayedaiwa kuvunja sheria wakati wanajeshi hao walipokuwa nchini humo miongo kadhaa iliyopita.

Ubalozi wa Uingereza nchini Kenya uliiambia BBC kuwa unafahamu shauri hilo na kwamba unanuia kutoa ushirikiano kwa wachunguzi.

Mamia ya watu wiki hii wamemiminika katika mikutano minne ya hadhara iliyofanyika karibu na kambi ya Batuk ili kusikiliza simulizi zenye hisia kuhusiana na madai ya utovu wa nidhamu wa wanajeshi wa Uingereza.

Memusi Lochede alielezea jinsi maafisa wa Uingereza waliahidi kumtunza bintiye Chaula Memusi mwenye umri wa miaka 22, ambaye yuko kwenye kiti cha magurudumu baada ya kudaiwa kugongwa na lori la jeshi la Uingereza na kujeruhiwa mnamo Januari 2019.

"Walituma mwakilishi kuniambia kwamba hawataki kesi mahakamani na kwamba watamtunza binti yangu," mama huyo mwenye umri wa miaka 45 alitoa ushahidi mbele ya moja wapo wa vikao vilivyokuwa vikifanyika nje chini ya ukumbi wa Archers Post, ambapo jeshi la Uingereza hufanya mazoezi.

Chini ya makubaliano na serikali ya Kenya, hadi vikosi sita vya askari wa miguu kwa mwaka hufanya mazoezi ya wiki nane nchini Kenya.

Bi Lochede alisema walilipia bili za hospitali ya bintiye kwa miaka miwili, lakini walishindwa kulipa fidia kama walivyoahidi.

Lino Lemaramba aliambia BBC kuwa alishuhudia ajali hiyo na alishtuka kuona lori la jeshi la Uingereza likiondoka baada ya kugongana. Alisimama kumsaidia Bi Memusi.

"Lilikuwa lori aina ya Batuk, nilijaribu kulisimamisha lakini likaendelea kusonga," alidai.

"Lilikuwa tukio la kusikitisha, damu imetapakaa, mifupa yake ilipondwa ... watu waliogopa kumgusa," alisema, akielezea jinsi ilivyokuwa vigumu kumuinua kwenye gari lake na kumpeleka hospitali.

Ushuhuda mwingine wa kusikitisha katika kesi hiyo ulitoka kwa Generica Namoru mwenye umri wa miaka 28, ambaye alikuwa ameandamana na binti yake wa miaka mitano.

Aliwaambia wajumbe wa uchunguzi huo, ulioanzishwa na kamati ya ulinzi ya bunge la Kenya, kwamba alipata ujauzito alipokuwa katika uhusiano na mwanajeshi wa Uingereza Batuk.huko

Alipomjulisha kuwa ni mjamzito, alikatisha uhusiano na kuondoka Kenya, akamwacha alee mtoto peke yake. Waliendelea kuwasiliana kwa muda na akamwambia kuhusu kuzaliwa kwa binti yao, lakini mawasiliano hayakuendelea tena.

"Ninachotaka tu ada ya matunzo ili mtoto wangu aweze kwenda shule na kuwa na maisha bora ya baadaye," alisema.

Vikao hivyo pia vilisikia ushahidi kutoka kwa msururu wa watu ambao walisema walikuwa na matatizo makubwa ya kiafya kufuatia moto unaodaiwa kuwashwa na wanajeshi wa Uingereza wakati wa mazoezi yaliyokuwa yakiandaliwa katika hifadhi ya wanyamapori mwaka 2021.

Moto huo unaosemekana kudumu kwa siku nne, uliharibu zaidi ya ekari 12,000 za ardhi na kusababisha mtu mmoja kupoteza maisha.

Lipaso Legei aliyekuwa amevalia vazi la kitamaduni la kimasai katika kikao hicho, alieleza kuwa aliponea kifo baada ya kuvamiwa na simba aliyekuwa akitoroka moto katika makazi yake ya asili.

“Nilivamiwa na simba karibu nifariki. Chini ya shuka hizi nina makovu ya majeraha mgongoni mwangu"

Aliongeza kuwa ukulima pia haujawezekana: "Hatuwezi kupanda mahindi, wanyama wanaendelea kuvamia, mbwa wetu wamevamiwa na fisi na chui."

Watu kadhaa walisema walikuwa na matatizo makubwa ya kupumua na kuumwa na macho. Simon Kaburu aliwasilisha rekodi zake za matibabu kwa wabunge na kueleza kwamba alilazimika kuwa na dawa za kukabiliana na "matatizo ya kifua baada ya kuvuta moshi".

Zaidi ya watu 7,000 wa eneo hilo wanaaminika kuanza hatua za kisheria dhidi ya jeshi la Uingereza kufuatia moto huo.

Uchunguzi huo kwa kiasi kikubwa umechochewa na kesi ya kushangaza ya Agnes Wanjiru.

Mwili wake ulipatikana kwenye tanki la maji taka mwaka 2012 baada ya kijana huyo mwenye umri wa miaka 21 kuonekana akiwa na kundi la wanajeshi wa Uingereza baada ya usiku wa kujivinjari .