Mlipuko wa lori la gesi Embakasi waibua maswali mengi

wananchi wataka serikali kuu na ya kaunti kufanya upelelezi kuhusu mikasa ya milipuko ya gesi ya mara kwa mara

Muhtasari
  • Watu wawil wameaga dunia baada ya gari lililokuwa likisafirisha gesi aina ya LPG kulipuka.
  • Visa vya mlipuko wa malori ya gesi vimekuwa vikishuhudiwa huku kisa cha leo kikiwa cha hivi punde
  • Ni wajibu wa serikali zote mbili kujishirikisha katika kutathmini usawa wa makampuni 
Moto Embakasi
Mkasa wa moto Embakasi Moto Embakasi
Image: Ezekiel Aming'a//THE STAR

Watu wawil wameaga dunia baada ya gari lililokuwa likisafirisha gesi aina ya LPG kulipuka.

“so apparently ni gari ilikuwa imebeba magari then kuna yenye ilikuwa inaleak ndani so huyo mubaba mwenye alikuwa anaendesha akaenda kunusa sijui hakusikia ama ni LPG hatukufika huko karibu. Akaenda kuwasha gari, kueka ignition ndio hiyo, ikalipuka.” Ndiyo iliyokuwa sauti ya shahidi.

Msongamano mkubwa wa magari umeshuhudiwa katika eneo la Outering road karibu na Fedha Avenue 1 kwenye eneo bunge la Embakasi Magharibi.

Aidha mlipuko huo umewawacha wengi wakiwa wamebung’aa kwani visa hivi vya mlipuko wa malori ya gesi vimekuwa vikishuhudiwa huku kisa cha leo kikiwa cha hivi punde.

“Tunaomba serikali kuu na serikali ya kaunti ziingilie kati katika kufanya uchunguzi wa kina kuhusu visa hivi vya milipuko ya gesi kwani ni suala linaloanza kuwa la mazoea sana."

"Vilevile, ni wajibu wa serikali zote mbili kujishirikisha katika kutathmini usawa wa makampuni haya iwapo yana vibali vinavyostahili na kustahiki katika uendeshaji wa operesheni zao ili kusiweze tokea mikasa mingine zaidi ya milipuko ya gesi,” alisema Victor Kulundu.

Naam, wananchi wameagizwa kuchukua hatua mwafaka hasa mikasa kama hii inapotokea. Vilevile, hali hii imezidi kuibua hisia mbalimbali huku wengi wakihofia hali yao ya usalama.

“Si kawaida kwa sababu mikasa hii inazidi kutokea moja baada ya nyingine. Hii si kawaida hasa katika eneo la Embakasi. Serikali ifanye uchunguzi wa kina na upelelezi zaidi ili tujue niaje milipuko hii inazidi kutokea moja baada ya nyingine kama misururu,” alisema Chris Ambutsi.

Mpaka sasa haijang’amuliwa ni watu wangapi wamejeruhiwa na shughuli za uokozi bado zinaendelea kufanyika katika eneo hilo la mkasa huu.