Ofisi ya Rais Mstaafu Uhuru yaweka mambo wazi kuhusu marupurupu yake

Kati ya Sh655 milioni zilizotengewa afisi hiyo katika mwaka wa kifedha wa 2022/2023, ofisi hiyo sasa inadai kuwa imepokea Sh28 milioni pekee.

Muhtasari
  • Katika hotuba kwa wanahabari Jumatatu iliyolenga kuweka rekodi sawa kuhusu hali ya mambo, msemaji wa ofisi hiyo Kanze Dena alidai kuwa rais huyo wa zamani amenyimwa pesa.
Rais mstaafu Uhuru Kenyatta
Rais mstaafu Uhuru Kenyatta
Image: Hisani

Ofisi ya rais wa nne Uhuru Kenyatta imeibua wasiwasi kutokana na kile ilichodai kushindwa kwa utawala wa rais William Ruto kushughulikia mahitaji yake ya kikatiba.

Katika hotuba kwa wanahabari Jumatatu iliyolenga kuweka rekodi sawa kuhusu hali ya mambo, msemaji wa ofisi hiyo Kanze Dena alidai kuwa rais huyo wa zamani amenyimwa pesa.

Kati ya Sh655 milioni zilizotengewa afisi hiyo katika mwaka wa kifedha wa 2022/2023, ofisi hiyo sasa inadai kuwa imepokea Sh28 milioni pekee.

"Hiyo ni takriban asilimia 4.4 ya bajeti yote ya mwaka huo," Kanze alisema.

Ofisi ya rais mstaafu Uhuru Kenyatta pia imekanusha ripoti kwamba serikali ilinunua magari mapya kwa ajili ya afisi yake kama inavyotakiwa na katiba.

Katika kikao na wanahabari, Uhuru kupitia kwa msemaji wake Kanze Dena badala yake alisema kwa sasa anatumia magari aliyopewa kwa njia ya mpito.

Kanze alisema magari yanayotumika ni yale ambayo Uhuru aliondoka nayo kutoka Kasarani baada ya hafla ya kukabidhi gari mnamo Septemba 2022.

"Baada ya mabadiliko hayo, mazungumzo kuhusu ununuzi wa magari hayo kama inavyotakiwa na Sheria yalianza kati ya ofisi hizo mbili...," Kanze alisema.

Akizungumza wakati wa kikao na wanahabari, Kanze alisema serikali pia imekataa kuwaongezea kandarasi wafanyakazi wawili.

Wafanyakazi aliosema ni Kanze Dena Mararo na msimamizi John Kariuki.

"Ofisi bado inasubiri uthibitisho na mawasiliano juu ya kwa nini walikataa kwa uwazi kuorodhesha kandarasi za wafanyikazi hawa wawili wa kitaalam," alisema.

Aidha alisema serikali haijafanya wala kuwezesha ukarabati wowote, matengenezo ya gari lolote wala haijatumia mafuta ya gari chini ya ofisi hii.