Mbunge wa Mumias Mashariki, Peter Salasya, amelazimika kufanya uamuzi kuhusu mswada wa kifedha wa mwaka 2024 baada ya kupokea simu nyingi kutoka kwa maelfu ya wakenya.
Salasya alisema kuwa alipigiwa simu na takriban wakenya 5,000 wakimsihi asikubaliane na mswada huo.
Mawasiliano haya yalikuwa sehemu ya mpango wa wakenya, ambapo nambari za simu za wabunge zilishirikiwa hadharani na wananchi waliombwa kuwasiliana na wabunge wao ili kudai wakatae mswada huo wa kifedha.
Salasya aliwaambia wakenya kwamba kura yake pekee haina uzito na kwamba waache kumpigia simu.
"Kutoka kwenye nafasi yangu, hata kama sitaki kukubaliana na mswada, wanasiasa wa Kenya Kwanza watakubaliana nao kwa kuwa wana idadi kubwa ya wabunge," alisema Salasya.
Aidha, alisisitiza kuwa simu hizo zilipaswa kuelekezwa kwa wabunge waliochaguliwa wa mrengo wa Kenya Kwanza.
"Kuna takriban nambari 5,000 zinazoniita, na baadhi yao ni wafuasi na mashabiki wa Kenya Kwanza ambao walimpigia kura Rais William Ruto. Mbona mnisumbue wakati mimi ni mwanachama wa Azimio?" aliuliza Salasya.
Salasya pia aliongeza kuwa mswada huo umeandaliwa na wanachama wa Kenya Kwanza na ni vyema wakenya wawapigie simu wabunge wa Kenya Kwanza.
"Wampigie Ruto na wamuulize kwa nini alileta mswada huo kwa Wakenya!" aliendelea.
Alimalizia kwa kusema, "Watu wanaonipigia wasinisumbue. Waelekeze maoni yao kwa Kenya Kwanza kwani ni wao ndio wataamua nini kitakachotokea."
Wakenya wengi wamejitokeza kupinga mswada huu ambao unaelekeza kuongezwa kwa kodi hasa wanapopambana na gharama ghali ya maisha.