Mataifa 5 yawatahadharisha raia wao dhidi ya hali tete Kenya

Mataifa hayo ni Urusi, Marekani ,Uingereza, Australia na India

Muhtasari

•Ubalozi wa Marekani uliwaonya raia wake kuepuka mikusanyiko mikubwa na kudumisha utulivu nchini Kenya.

•Pia walishauriwa kufuatilia vyombo vya habari vya ndani ya nchi kwa habari zaidi 

•Uingereza iliwashauri raia wake kuchukua tahadhari wanapotembelea maeneo maalum kama Mandera, Lamu, Tana River, na Kisiwa cha Manda.

Waandamanaji Nairobi
Image: JOSEPH OMBATI

Nchi tano zimetoa tahadhari za safari kwa raia wao nchini Kenya kutokana na maandamano dhidi ya Mswada wa Fedha.

Vijana wa Kenya walivamia majengo ya bunge huku wakiitaka serikali kufutilia mbali Mswada wa Fedha wa 2024, wakilalamikia ongezeko la ushuru uliokuwa ghali na ukosefu wa uwajibikaji kwa utawala wa sasa.

Hali hii ilisababisha mapambano kati ya polisi na waandamanaji ambao walijibu kwa kuwapiga risasi raia.

Kulingana na Amnesty International, zaidi ya wakenya 13 walipigwa risasi  siku ya Jumanne huku  wengine wakiuguza majeraha katika hospitali za nchini.

Ubalozi wa Marekani uliwaonya raia wake kuepuka mikusanyiko mikubwa na kudumisha utulivu nchini Kenya.

Pia walishauriwa kufuatilia vyombo vya habari vya ndani ya nchi kwa habari zaidi na kuwa na kitambulisho sahihi ikiwemo nakala ya pasipoti yao ya Marekani na visa yao ya Kenya ya sasa.

"Maandamano yaliyopangwa kuhusu kupinga Mswada wa Fedha wa 2024 yanatarajiwa kuendelea. Hasa, kuna wito wa maandamano katika sehemu ya katikati mwa jiji la  Nairobi na miji mingine kote Kenya siku ya Jumanne, Juni 25, na Alhamisi, Juni 27," ilisema sehemu ya taarifa hiyo.

"Walakini, mikusanyiko mikubwa ya umma inaweza kugeuka kuwa ya vurugu wakati wowote na kusambaa kwenye sehemu kadhaa za jiji. Inapendekezwa kuwa ange na kuepuka mikusanyiko mikubwa. Matatizo ya trafiki yanatarajiwa."

Kwa upande wake, Uingereza iliwashauri raia wake kuchukua tahadhari wanapotembelea maeneo maalum kama Mandera, Lamu, Tana River, na Kisiwa cha Manda.

Serikali ya Australia pia ilitoa tahadhari, ikionya raia wake kuepuka maeneo yanayoweza kushambuliwa na kubaki macho wanapotembelea maeneo ya umma.

Ubalozi wa Urusi nchini Kenya pia uliwaomba raia wake kuepuka maeneo yenye mikusanyiko ya watu katika miji ya Nairobi, Mombasa, Kisumu, Kakamega, Eldoret, Nakuru, Nanyuki, Nyeri, Kisii, Kilifi, Embu, na Kericho katika siku zijazo.

Balozi ya India nchini Kenya pia iliwashauri raia wake kuchukua tahadhari na kuzuia harakati zisizo za lazima wakati wa maandamano vilevile kuepuka maeneo yanayoweza kushambuliwa hadi hali itakapokuwa tulivu na shwari.