Gavana Orengo amtaka rais Ruto na serikali yake kujiuzulu

Kiongozi huyo alidai kuwa wakenya hawana imani na utawala wa rais.

Muhtasari

•"Kuzungumza naye hakutasuluhisha chochote kwani kuna hasira nyingi dhidi ya uongozi wa Kenya Kwanza. Kama yeye ni mkristo , ajiuzulu na serikali yake yote,” alisema Orengo mnamo Jumapili.

•Akizungumza eneo la Bondo, gavana huyo alisema katika makadirio yake kuwa serikali ya Kenya Kwanza imewafeli wakenya na kwamba inafaa ijiuzulu mamlakani kwa ujumla.

Gavana wa Siaya James Orengo
Gavana wa Siaya James Orengo Gavana wa Siaya James Orengo
Image: HISANI

Gavana wa  Siaya James Orengo amemtaka Rais William Ruto kujiuzulu kutokana na ukosoaji na hamaki nyingi kutoka kwa wananchi inayoelekezwa kwa serikali ya Kenya Kwanza.

Anasema kuwa, iwapo Rais Ruto hatasikiliza malalamishi ya wananchi, basi itambidi ajiuzulu kwa kuwa madai kuwa wakenya wamechoka na utawala wa sasa.

“Kama Ruto hatatilia maanani malalamishi ya wakenya, kuzungumza naye hakutasuluhisha chochote kwani kuna hasira nyingi dhidi ya uongozi wa Kenya Kwanza. Kama yeye ni mkristo , ajiuzulu na serikali yake yote,” alisema Orengo mnamo Jumapili.

Akizungumza katika eneo la Bondo, gavana huyo alisema katika makadirio yake kuwa serikali ya Kenya Kwanza imewafeli wakenya na kwamba inafaa ijiuzulu mamlakani kwa ujumla.

“Tunaweza pata usaidizi kutoka kwa taasisi za kimataifa kama vile mnamo 2002 na 2007 ili tulete harakati mpya ambazo zitawezesha mpito wetu kutoka kwa serikali hii ya kiimla hadi utawala mpya,” Orengo alisema.

Kufuatia kuondolewa kwa mswada tata wa fedha 2024 baada ya maandamano makali nchini- ambayo Ruto ameonya kuwa Kenya itarudi katika ukopaji ili kukidhi mahitaji yake- Orengo alisema kuwa wakenya wajiandae kwa nyakati za mbele.

Orengo alizingatia kuwa huduma za serikali zitapunguka mno.

Rais ruto mnamo Jumapili aliwekeza taswira tata ya nchi kufuatia kukataliwa kwa mswada wa fedha akisema  kuwa Kenya itarudi nyuma kwa miaka miwili na itahitaji kukopa takriban trilioni 1.2 mwakani ili serikali ifanye kazi.

Vilevile, aliwaambia watangazaji kuwa kuukataa mswada huo inamaanisha serikali itakuwa na ugumu wa, kwa mfano, kuthibitisha walimu 46,000 wa Shule ya Sekondari ya Vijana kwa misingi ya kudumu na ya pensheni.

Mswada wa fedha 2024 ulikuwa umependekeza kuongezwa kwa tozo kwani serikali ya Rais Ruto ilikuwa imetaka kuinua mapato kwa shilingi bilioni 346.7 kwa bajeti ya mwaka 2024/25.