Vijana 12 wakamatwa kwa madai ya kuvamia kituo cha polisi Bondo

Walianza kushambulia kituo cha polisi baada ya maandamano ya yaliyopangwa Alhamisi kufeli

Muhtasari

•Vijana hao walianza kukusanyika katika mji wa Bondo masaa ya saa sita adhuhuri huku wakijaribu kufunga barabara za uchukuzi kutoka eneo hilo.

•Timu hiyo ya kupambana na ghasia ilisalia ange na kidete huku wakizidi kushika doria mjini kwa minajili ya kuwatawanya waandamanaji wadogo wadogo mpaka majira ya saa tatu jioni

vIJANA 12 watiwa mbaroni kwa kushambulia kituo cha polisi
Image: HISANI

Vijana 12 wametiwa mbaroni kwa madai ya kujaribu kuvamia kituo cha polisi cha Bondo baada ya maandamano ya kupinga serikali kutokuwepo mnamo Alhamisi kama ilivyopangwa.

Kulingana na Kamanda wa polisi wa kaunti ya Siaya, Cleti Kimaiyo, vijana hao walianza kukusanyika katika mji wa Bondo masaa ya saa sita adhuhuri huku wakijaribu kufunga barabara za uchukuzi kutoka eneo hilo.

Kamanda huyo alidokeza kuwa wakati was aa nane adhuhuri, kundi dogo la waandamanaji walianza kuvamia kituo cha polisi huku wakirusha mawe mighairi ya kuacha.

Mbali na hayo, alisema kuwa,  tukio hili liliwalazimu timu ya kupambana na ghasia ikiongozwa naye kujibu vurumai ya vijana hawa.

Aidha, juhudi na jitihada za polisi hawa ziligonga ndipo kwani, walifanikiwa kuwatawanya kabisa waandamanaji hao wa vurugu kutoka kwenye mji.

Bwana Kimaiyo vilevile, aliongezea kuwa, walifanikiwa kuwakamata washukiwa 12 ambao walikuwa wanavamia kituo hicho kwa mawe na njia nyingine za vurugu.

Mkuu huyo wa polisi kwenye kaunti hiyo alizungumzia kuwa timu hiyo ya kupambana na ghasia ilisalia ange na kidete huku wakizidi kushika doria mjini kwa minajili ya kuwatawanya waandamanaji wadogo wadogo.

Ilipowadia majira ya saa tatu jioni, operesheni hii ilifikia kikomo huku amani na utulivu ikishuhudiwa katika mji wa Bondo.

Fauka ya hayo, aliongezea kuwa, hamna watu waliojeruhiwa kwani hakukuwa na ripoti zilizofikishwa kwenye kambi.

Alisisitiza kuwa vijana waliohusika watafikishwa mahakamani mnamo Ijumaa na sheria itatekeleza mkondo wake.