Maafisa wastaafu wa jeshi la ulinzi la kenya chini ya mwavuli (Kenya Veterans for Peace) wameitaka serikali kuingilia kati na kuhakikisha wanajeshi wa zamani wa KDF wanaishi maisha ya starehe.
Akizungumza alipowatembelea Wanajeshi wa zamani wa KDF, Afisa Mkuu Mtendaji wa Veterans For Peace, Dkt Nelson Sechere alisema Wanajeshi hao wa Zamani walitumikia nchi kwa bidii na hawafai kusahaulika.
Maveterani hao walitoa usaidizi kwa wenzao waliostaafu na familia za maafisa waliofariki katika kaunti ya Machakos.
Waligawa vyakula vya aina mbalimbali kwa familia za wenzao waliokufa wakiwa kazini ili kuwahudumia katika nyakati ngumu za kiuchumi.
Dkt Sechere alisema wanalenga maeneo yote, na pia wanachimba visima kadhaa ili kuchangia usalama wa chakula nchini.
Luteni kanali mstaafu Moses Sande, mnufaika wa mpango wa chakula anasema waliunda shirika hilo baada ya ghasia za baada ya uchaguzi wa 2008 ili kutetea amani miongoni mwa jamii tofauti.