DCI kuchunguza madai ya ununuzi wa bastola iliyotumika kumuua Tom Mboya

Uchunguzi huu unaanza baada ya mwanaume wa miaka 92 kudai kuwa alinunua bastola hiyo.

Muhtasari

• Idara ya Uchunguzi wa Jinai imeelekezwa kwenye makala kwamba mwanaume mwenye umri wa miaka 92 alinunua bastola iliyotumika katika mauaji ya Tom Mboya.

•Tom Mboya, alikuwa kiongozi muhimu katika harakati za uhuru wa Kenya na serikali ya baada ya ukoloni, aliuawa tarehe 5 Julai, 1969.

Picha ya hayati Tom Mboya
Image: HISANI

Idara ya Uchunguzi wa Makosa ya  Jinai (DCI) imeanzisha uchunguzi baada ya ripoti kuwa mwanaume mwenye umri wa miaka 92 alidaiwa kununua bastola iliyotumika katika mauaji ya Tom Mboya.

"Uangalizi wa Idara ya Uchunguzi wa Jinai umeelekezwa kwenye ripoti kwamba mwanaume mwenye umri wa miaka 92 alinunua bastola iliyotumika katika mauaji ya Tom Mboya.

Alikuwa mwanachama wa vyama vya wafanyakazi, mwalimu, Mpanafrika, mwandishi, waziri wa zamani na mwanasiasa," ilieleza DCI.

"DCI imeanzisha uchunguzi na hatua muhimu zitachukuliwa mara uchunguzi utakapokamilika."

Tom Mboya,alikuwa kiongozi muhimu katika harakati za uhuru wa Kenya na serikali ya baada ya ukoloni, aliuawa tarehe 5 Julai, 1969.

Akiwa na umri wa miaka 30, Mboya alikuwa mwanachama mwanzilishi wa Chama cha Kenya Africa National Union (KANU).

Alikuwa Waziri wa Sheria na Mambo ya Katiba katika utawala wa kwanza wa Jomo Kenyatta na baadaye akahudumu kama Waziri wa Mpango na Maendeleo ya Kiuchumi.

Mauaji ya Mboya yalikuwa na athari kubwa kwa Kenya na bara la Afrika kwa ujumla, kwani alikuwa mtetezi wa umoja wa bara la Afrika na maendeleo ya kiuchumi.

Uchunguzi huu wa DCI unalenga kuchunguza mchakato wa ununuzi wa silaha iliyotumika katika tukio hilo la kusikitisha, na ni hatua muhimu katika kutafuta haki na kufichua ukweli wa kihistoria wa tukio hilo la kusikitisha la mauaji ya Tom Mboya.