Kalonzo amsihi Rais kusikiliza maoni ya Genz asije akabanduliwa

Vilevile, amemtaka rais amfute Insepkta Jenerali wa polisi kufuatia mauaji ya vijana 42

Muhtasari

•“Tusipokuwa makini wote tutatupwa nje na Gen Z kwa sababu wanasema wamehitimu umri... " Alisema Kalonzo.

•"Agiza IG Japeth Koome ajiuzulu na kuwajibikia vifo vya vijana 42 wa Kenya waliopoteza maisha kwa sababu walikuwa wakitekeleza haki yao ya kikatiba,"aliendelea Kalonzo

KALONZO MUSYOKA
Image: HISANI

Kiongozi wa Chama cha Wiper Kalonzo Musyoka ameonya kuwa Rais William Ruto anafaa kuzingatia kwa uzito maswala yaliyoibuliwa na vijana wa Kenya.

Akizungumza KICC, huku Rais Ruto akitia saini mswada wa IEBC kuwa sheria, Kalonzo alieleza kuwa walinzi hao wazee wasipokuwa makini,huenda vijana wa Kenya hasa Generation Z wakawaondoa mamlakani.

“Tusipokuwa makini wote tutatupwa nje na Gen Z kwa sababu wanasema wamehitimu umri... mnasema sisi ni viongozi wa kesho ila sisi ni viongozi wa sasa na hatuwezi kuwatupa mbali. " Kalonzo alionya.

Makamu huyo wa rais wa zamani aliomba Ruto aharakishe mapendekezo ya ripoti ya NADCO, ambayo ilitayarishwa na kamati aliyoongoza pamoja, akitaja kuidhinishwa kwa sheria ya mswada wa IEBC kuwa mojawapo ya mapendekezo.

"Agiza IG Japeth Koome ajiuzulu na kuwajibikia vifo vya vijana 42 wa Kenya waliopoteza maisha kwa sababu walikuwa wakitekeleza haki yao ya kikatiba ya kukusanyika kwa amani na kuandamana kwa amani.

Mheshimiwa Rais, Jeshi linafaa kuagizwa kutoka mitaani kwetu na kutumwa. kurudi kwenye kambi," aliongeza.

Zaidi ya hayo, Kalonzo alimtaka Ruto kumpiga kalamu Inspekta Jenerali wa Polisi Japheth Koome kufuatia mauaji ya watu 42 wakati wa maandamano ya amani.

Onyo la Kalonzo linakuja baada ya wiki kadhaa za maandamano ya mitaani yanayoongozwa na vijana kupinga Mswada wa Sheria ya Fedha wa 2024 na kudai uwajibikaji kutoka kwa serikali.

Kilele cha maandamano hayo kilishuhudia waandamanaji wakivunja bunge na kuliteketeza kiasi cha kusababisha waandamanaji kadhaa kupigwa risasi na vikosi vya usalama.

Maandamano hayo yalimfanya Ruto kukataa mswada huo kwa jumla, na kuahidi kutekeleza hatua za kubana matumizi ili kupunguza matumizi ya serikali.