Wakulima wa Mwea walilia kuhusu uvamizi wa panya

Wanarai serikali kuwekeza mikakati mwafaka ili kupambana na panya hao

Muhtasari

•Panyabuku hao wanaweza kuathiri ukuaji wa mchele ambao ndio mmea unaokuzwa zaidi katika eneo hilo.

• wanakabiliana na panya hao kwa kutumia njia za zamani kama vile uwashaji mishumaa  kwenye mashamba ya mchele usiku ili kuwashtua na kuwatorosha panya hao kutoka kwenye mashamba

Picha ya panya
Picha ya panya
Image: BBC

Wakulima wa mchele katika eneo la Mwea Tebere wanakadiria hasara baada ya panyabuku kushambulia mimea (mchele)  yao shambani.

Wakulima, wakiongozwa na John Munene na Pius Njogu kutoka sehemu ya Thiba, walisema kuwa panyabuku hao wanaweza kuathiri ukuaji wa mchele ambao ndio mmea unaokuzwa zaidi katika eneo hilo.

Vilevile, wanahofia kuwa panya hao ni hatari kwenye usalama wa chakula katika nchi.

Wakulima hao wa mchele wanakabiliana na panya hao kwa kutumia njia za zamani kama vile uwashaji mishumaa  kwenye mashamba ya mchele usiku ili kuwashtua na kuwatorosha panya hao kutoka kwenye mashamba yao.

Mbali na hayo, wanasihi serikali iingilie kati ili kupata suluhu mwafaka kwa kizaazaa hiki kinachozidi kuwa hatari kwenye maisha ya binadamu.

Kulingana na Munene,  wakulima wa mchele wanakadiria mazao hafifu baada ya uvamizi wa konokono mapema mwaka huu huku sasa wakishambuliwa na panyabuku.

“Ni mwaka wa pili tangu panya kuvamia mashamba haya na imekua zaidi ya miaka mitano tangu konokono kuvamia skimu hii Mwea. Nani sasa atasaidia wakulima wa Mwea?” Aliuliza Munene.

Pius Njogu, kwa upande wake, alisema kuwa panya hao wanazaana kwa haraka na kwamba hawawapi wakulima wa mchele usingizi.

“Ni baridi mno kwani tunatumia nguvu zetu kupigana na panya hawa. Nani atatusaidia?” Njogu alimalizia.