- Kaimu Inspekta Jenerali wa Polisi Douglas Kanja alitangaza maafisa hao watachukuliwa na timu mpya hata uchunguzi kuhusu tukio hilo ukiendelea.
Maafisa wote wa polisi walio katika Kituo cha Polisi cha Kware katika mtaa wa mabanda wa Mukuru, Nairobi ambapo takriban miili minane ya wanawake imepatikana wamehamishwa.
Kaimu Inspekta Jenerali wa Polisi Douglas Kanja alitangaza maafisa hao watachukuliwa na timu mpya hata uchunguzi kuhusu tukio hilo ukiendelea.
Alifichua hayo Jumapili, Julai 14 huku maafisa wakiendelea kutafuta miili zaidi katika machimbo yaliyotelekezwa katika eneo hilo lenye watu wengi.
Kanja alisema hatua hiyo inalenga kuhakikisha uchunguzi wa haki na usawa.
Kanja alisema uchunguzi wa awali unaonyesha kuwa maiti zote nane zilizopatikana kwenye jalala la Kware zilikuwa za kike na ziliagwa vibaya.
"Nairobi Funeral Home kwa sasa inahifadhi miili minane. Uchunguzi unaonyesha kuwa miili yote iliyopatikana ilikuwa ya wanawake ambayo ilikatwa vipande vipande na katika hali tofauti ya kuoza," alisema.
Itachukua siku 21 polisi na mashirika ya uchunguzi kutegua kitendawili cha miili iliyoagwa iliyopatikana katika jalala la Kware, eneo bunge la Embakasi Kusini, Kanja alisema.
Kaimu IG aliendelea kusema wale wote waliohusika watawajibishwa baada ya uchunguzi.
"Katika wakati huu mgumu, tunasimama na jamii na kubaki na dhamira ya kufichua ukweli na kuwafikisha waliohusika kwenye vyombo vya sheria. Tukumbuke hawa ni maisha ya watu waliopotea na wana familia," alisema.
"Tunatoa wito kwa umma kuepuka uvumi wowote na kutoa nafasi kwa uchunguzi."
Aliwataka umma kushirikiana na kujitolea habari na kitengo cha uchunguzi wa mauaji katika DCI au kuripoti kwa kituo cha polisi kilicho karibu.