logo

NOW ON AIR

Listen in Live

"Hili nayo itapita!" Gavana Mwangaza avunja kimya baada ya kung'atuliwa kwa mara ya 5

Pia alijitia moyo kwa mstari wa Biblia kutoka kitabu cha Zaburi sura ya 34 unaozungumzia ulinzi wa Mungu

image
na Samuel Maina

Habari09 August 2024 - 05:11

Muhtasari


  • •Akizungumza baada ya hatua hiyo, gavana Mwangaza alibainisha kuwa kubanduliwa kwa mara ya tano pia kutafeli hatimaye.
  • •Mwanasiasa huyo pia alijitia moyo kwa mstari wa Biblia kutoka kitabu cha Zaburi sura ya 34 unaozungumzia ulinzi wa Mungu.

Gavana wa Meru, Kawira Mwangaza ameelezea imani yake kubwa ya kunusurika tena baada ya kung’atuliwa madarakani kwa mara ya tano.

Siku ya Alhamisi, MCAs wa Meru walipiga kura ya kumtimua gavana, na kumfanya kuwa kiongozi wa kwanza wa kaunti kubanduliwa mara kadhaa.

Akizungumza baada ya hatua hiyo, gavana Mwangaza alibainisha kuwa kubanduliwa kwa mara ya tano pia kutafeli hatimaye.

"Kubanduliwa kwa mara ya 5? Hili nalo litapita! Gavana ni Mama,” Kawira alisema kupitia Facebook.

Siku ya Ijumaa asubuhi, mwanasiasa huyo alijitia moyo kwa mstari wa Biblia kutoka Zaburi sura ya 34 unaozungumzia ulinzi wa Mungu.

“Bwana Mungu atatupa utajiri wa kimungu. Malaika wa Bwana atapiga kambi kutuzunguka na kutuokoa na maovu yote. Tutafurahia baraka tele. Tutapata upendeleo usio wa kawaida na usaidizi ambao haujaombwa.

Mwenyezi Mungu hakika atafanya maajabu katika maisha na kaya zetu. Tutakula matunda ya kazi yetu. Bwana Mungu atatulinda na kutuweka salama. Atatushangaza na kufanya kila kitu kifanye kazi kwa ajili yetu. Tutarithi utajiri wa mataifa katika Jina la Yesu Kuu,” gavana huyo aliandika.

Alhamisi, gavana Mwangaza alitimuliwa kwa mara ya tano katika kipindi cha miaka miwili baada ya MCAs kupiga kura kuunga mkono hoja ya yeye kuondolewa madarakani.

Mwangaza alibanduliwa ofisini baada ya MCAs 49 kupiga kura kuunga mkono hoja dhidi ya 17 walioikataa.

Wajumbe watatu walikosa kujitokeza katika mkutano huo wa kura ya kumuondoa madarakani.

Mwangaza atasubiri uamuzi wa Seneti kufahamu iwapo bunge hilo litamwokoa au kuunga mkono kubanduliwa kwake.

Anakuwa gavana wa kwanza kubanduliwa mara kadhaa nchini.

MCA wa kuteuliwa Zipporah Kinya alimshutumu Mwangaza kwa makosa matatu: ukiukaji mkubwa wa katiba, utovu wa nidhamu na matumizi mabaya ya ofisi.

Katika ukiukwaji mkubwa wa katiba na sheria zingine, Kinya alisema Mwangaza alitengua uteuzi wa Virginia Kawira kama katibu wa bodi ya utumishi wa umma kaunti hiyo.

"Ni bunge la kaunti pekee ndilo lililo na mamlaka ya kubatilisha uteuzi wa katibu wa bodi ya utumishi wa umma katika kaunti," alisema.

Naibu kiongozi huyo alisema Mwangaza alikosa kuwateua Wenyeviti wa Bodi ya Mapato ya Kaunti ya Meru, Meru Microfinance Corporation, Bodi ya Huduma kwa Vijana ya Meru, na Bodi ya Shirika la Uwekezaji na Maendeleo ya Kaunti ya Meru kama inavyotakiwa kisheria hivyo kushindwa kuzifanyia kazi Bodi hizo.

Aliendelea kueleza kuwa Mwangaza alikataa kutekeleza mapendekezo na maazimio ya Bunge la Kaunti yaliyomtaka gavana kuwafuta kazi Katibu wa Kaunti, Kiambi Athiru Thambura, na Mkuu wa Wafanyikazi, Harrison Gatobu Nchamba Mbithi kutoka ofisini kwa ukiukaji mkubwa wa sheria za Katiba. .

Alisema  Kiambi Athiru na mkuu wa wafanyikazi Harrison Gatobu pia wamekuwa wakiwaajiri na kuwafuta kazi kinyume cha sheria lakini Mwangaza hakuchukua hatua yoyote.

Bado katika shtaka hilo la ukiukwaji mkubwa wa katiba na sheria nyingine, Kinya alimshutumu Mwangaza kwa kumfukuza kazi kinyume cha sheria Dk Ntoiti (Mkurugenzi Mtendaji wa Bodi ya Mapato ya Kaunti), Paul Mwaki (Mkurugenzi Mtendaji wa Bodi ya Vileo), Kenneth Kimathi Mbae (Mkurugenzi Mkuu wa Meru Microfinance Corporation), na Joseph Kithure Mberia (Mkurugenzi Mtendaji, MEWASS) katika unyakuzi wa mamlaka ya mamlaka za uteuzi kinyume na kifungu cha 9 (7)(b) cha Sheria ya Bodi ya Mapato ya Kaunti ya Meru na kifungu cha 10(6) cha Shirika la Uwekezaji na Maendeleo la Kaunti ya Meru.

Kutokana na hatua hiyo, Kinya alisema Serikali ya Kaunti ya Meru imekabiliwa na gharama na fidia ya Sh4 milioni na Mahakama ya Ajira na Mahusiano ya Kazi.


RADIO JAMBO FREQUENCIES

Kisumu 100.1 | Mombasa 92.3 | Nakuru 96.9 | Eldoret 99.5 | Nyeri 99.3 | Nyahururu 97.3 | Webuye 95.3 | Meru 92.7 | Kitui 104.9 | Kibwezi 104.7 | Voi 105.7 | Malindi 98.1 | Lamu 104.7 | Narok 97.3 | Kapenguria 99.7 | Kisii 89.3 | Garissa 104.3 | Maralal 97.3 | Lodwar 92.7


logo© Radio Jambo 2024. All rights reserved