RIP! Askofu aliyevuma kwa kuwagusa wanawake isivyofaa akidai 'kuwatoa pepo' afariki

Baba huyo wa watoto wanne alikuwa akipambana na ugonjwa wa Meningitis.

Muhtasari

•Mke wa Johanna, Mary Wanjiku alithibitisha kifo chake akifichua alikata roho katika hospitali ya Nakuru alipokuwa akipokea matibabu.

•"Mume wangu mpendwa na baba wa watoto wangu wanne alifariki akiwa na umri wa miaka 54 na tutakosa upendo wake," Mkewe alisema.

Image: HISANI

Askofu mwenye utata Danson Gichuhi almaarufu Johanna ameaga dunia!

Johanna ambaye alivuma sana mapema mwaka huu baada ya video kuibuka zikimuonyesha akiwagusa waumini wa kike kwa njia isiyofaa kwa jina la kufukuza pepo wabaya alifariki siku ya Alhamisi baada ya kupambana na ugonjwa kwa muda mrefu.

Mke wa Johanna, Mary Wanjiku alithibitisha kifo chake akifichua kwamba alikata roho katika hospitali ya Nakuru alipokuwa akipokea matibabu.

"Mume wangu mpendwa na baba wa watoto wangu wanne alifariki akiwa na umri wa miaka 54 na tutakosa upendo wake, ari na bidii yake, kando na kuwa nguzo yetu ya kiroho," alisema Bi Wanjiku aliambia NTV.

Inaripotiwa kuwa baba huyo wa watoto wanne alikuwa akipambana na ugonjwa wa Meningitis.

Februari mwaka huu, video za Askofu Johanna ‘akitoa pepo’ kutoka kwa wanawake kwa njia ya kutatanisha ziliibuka kwenye mitandao ya kijamii.

Johanna  alianza kuvuma baada ya video iliyomuonyesha akipaka mafuta kwenye sehemu mbalimbali za mwili wa mwanamke aliyelala chali kusambazwa kwenye mitandao mbalimbali ya kijamii.

Katika video hiyo, mtumishi huyo wa Mungu alisikika akimwombea mwanamke huyo huku akiendelea kumpaka mafuta mwilini.

Katika mahojiano na Kururia TV, Johanna alifichua kwamba ni mwanamke huyo aliyemtafuta ili amsaidie kukabiliana na masuala ya ndoa ambayo alikuwa akikabiliana nayo.

"Video ilichukuliwa Ijumaa. Mwanamke huyo alikuwa ametoka Nairobi. Alikuja na matatizo mengi ya ndoa. Mumewe alikuwa ametoroka na kumuacha na watoto watatu. Mumewe alikuwa amechukuliwa na mwanamke mwingine. Mwanaume huyo angerudi nyumbani mchana na baadaye kwenda tena,” Askofu Johanna alisimulia

Aliongeza. “Mume wake alipoenda sana, mwanamke huyo aliona namba yangu na kunipigia. Aliniambia kuwa anataka kuja kanisani kwangu ili niweze kumhudumia. Alipokuja nilimhudumia, niliona shida alizonazo (kawaida huwa naona shida za watu). Nikamwambia kuna mwanamke anayeitwa ‘Carol’ amemchukua mumewe. Carol ndiye mwanamke aliyempokonya mume wa mwanamke huyo. Bibi huyo anaitwa Wanjiru."

Huku akitetea mtindo aliotumia kufukuza mapepo, Johanna alitumia mstari wa Biblia kuhusu uhitaji wa mgonjwa kutafuta wazee wa kanisa ili wawapake mafuta kwa ajili ya uponyaji.