Similiki gari lililopatikana na vitoa machozi – Wanjigi

Wanjigi katika kesi iliyowasilishwa katika Mahakama ya Milimani anasema anasingiziwa andaliwa kwa sababu za kisiasa.

Muhtasari

• IG alimtaka Wanjigi kujisalimisha kwa polisi ili kuhojiwa.Wanjigi sasa anasema gari hilo si lake au la washirika wake kama ilivyoripotiwa awali. 

• Wanjigi ameiomba mahakama kumpa dhamana ya kutarajia dhidi ya hatua ya kukamatwa au kushtakiwa na polisi. 

Mfanyabiashara Jimmy Wanjigi amedai kuwa yeye si mmiliki wa gari linalodaiwa kupatikana na vitoa machozi wakati wa maandamano ya Nane Nane jijini Nairobi. 

Wanjigi katika kesi iliyowasilishwa katika Mahakama ya Milimani anasema anasingiziwa andaliwa kwa sababu za kisiasa. 

Katika kikao na wanahabari, kaimu Inspekta jenerali wa polisi Alhamisi alifahamisha umma kwamba walipata vitoa machozi vinne, chaja mbili za Motorola, simu moja ya miongoni mwa vifaa vingine kwenye gari lililoegeshwa kando ya lango la Wanjigi. 

Kutokana na kupatikana kwa vifaa hivyo, IG alimtaka Wanjigi kujisalimisha kwa polisi ili kuhojiwa.Wanjigi sasa anasema gari hilo si lake au la washirika wake kama ilivyoripotiwa awali. 

"Ninaamini kuwa IG hana sababu halali za kunikamata au kujiwasilisha kwenye kituo chochote cha polisi kama alivyodai au kupendekeza mashtaka ya jinai dhidi yangu," alisema. 

Kupitia kwa wakili Nelson Osiemo, Wanjigi ameiomba mahakama kumpa dhamana ya kutarajia dhidi ya hatua ya kukamatwa au kushtakiwa na polisi. Pia kinachotafutwa ni amri ya kumzuia IG kumkamata na kudhibiti haki zake kusafiri? 

"Katika kipindi cha miezi michache iliyopita, nimekuwa nikipatwa na msongo wa mawazo na kisaikolojia kwani maafisa wa polisi wamekuwa wakinitisha, kuninyanyasa na kunifuata nyuma," alisema. 

Anasema ana uhuru na haki yake ya faragha imeminywa kwa kisingizio kuwa anafadhili maandamano kote nchini.