Aliyekuwa Waziri Mkuu Raila Odinga amepata uungwaji mkono wa takriban nchi 19 katika kinyang’anyiro chake kuania uwenyekiti wa tume ya umoja wa Afrika.
Raila anajiandaa kuzindua kampeni kubwa barani Afrika kutafuta uungwaji wa mataifa mengine ya Afrika kwa nafasi hiyo.
Taarifa zinajiri wakati inaarifiwa kwamba Rais William Ruto anajiandaa kuzindua rasmi kampeni ya Raila kuwa mwenyekiti wa Tume ya Muungano wa Afrika siku ya Jumanne wiki ijayo.
Kinyang'anyiro hicho kinaonekana kuwa kibarua kikubwa cha kidiplomasia kwa Rais Ruto kwani atajaribu ushawishi wake miongoni mwa wenzake kote barani Afrika.
Raila anawania nafasi hiyo dhidi ya Mohamoud Youssouf wa Djibouti, Anil Gayan (Mauritius) na Richard Randriamandrato (Madagascar).
Wanne hao wanataka kumrithi mwenyekiti anayeondoka Moussa Faki wa Chad. Uchaguzi huo umepangwa kufanyika Februari mwaka ujao.
Mgombea wa Djibouti ambaye alizuru Nairobi kufanya kampeni wiki mbili zilizopita anaonekana kuwa mpinzani mkuu wa Raila.
Raila alitangaza kujiondoa kutoka siasa za humu nchini ili kuangazia kinyang’anyiro cha AUC.