logo

NOW ON AIR

Listen in Live

Rais Ruto aweka wazi kwa nini alilazimika kufanya kazi na upinzani

"Kuna wakati katika ustawi  wa taifa ambapo umoja wa taifa, maendeleo ya Kenya, mabadiliko ya taifa letu ni muhimu zaidi," alisema.

image
na Samuel Maina

Habari24 August 2024 - 12:39

Muhtasari


  • •Ruto alibainisha kuwa Kenya ilikuwa katika hali ya kipekee ambayo ililazimu kuweka kando maslahi ya kibinafsi au ya kisiasa.
  • •Ruto aliandamana na viongozi kadhaa akiwemo Waziri wa Kawi Opiyo Wandayi na mwenzake wa Ardhi Alice Wahome.
Rais William Ruto akiwa na Katibu wa waziri wa Nishati Opiyo Wandayi, Gavana wa Siaya James Orengo, seneta wa Uasin Gishu Jackson Mandago na Naibu Waziri wa Nishati Alex Wachira huko Aldai, Nandi mnamo Agosti 24, 2024.

Rais William Ruto ametetea uamuzi wake wa kuwahusisha viongozi wa upinzani katika serikali yake akisema ni muhimu kwa umoja wa taifa.

Ruto ambaye alikuwa akihutubia wakazi wa Kobujoi, eneo la Aldai, kaunti ya Nandi, alibainisha kuwa Kenya ilikuwa katika hali ya kipekee ambayo ililazimu kuweka kando maslahi ya kibinafsi au ya kisiasa.

"Kuna wakati katika ustawi  wa taifa ambapo umoja wa taifa, maendeleo ya Kenya, mabadiliko ya taifa letu ni muhimu zaidi kuliko ushawishi wowote wa kisiasa, pande za kisiasa, muundo wa kisiasa au maslahi yoyote ya jamii," alisema. alisema.

"Hata ni zaidi ya maslahi binafsi ya viongozi, lazima tuungane na huo ni wakati kama huu katika nchi yetu," aliongeza.

Ruto aliandamana na viongozi kadhaa akiwemo Waziri wa Kawi Opiyo Wandayi na mwenzake wa Ardhi Alice Wahome.

Magavana Stephen Sang (Nandi) na James Orengo (Kisumu) na wabunge kadhaa pia walikuwepo.

Mkuu huyo wa nchi alibainisha kuwa mabadiliko ya taifa yanawahitaji viongozi wote na Wakenya kwa jumla kuwa na umoja bila kujali misimamo yao ya kisiasa.

Alikuwa katika kaunti hiyo kukagua ujenzi wa soko la Kobujoi.

Inastahili kufunguliwa mnamo Desemba.

Hapo awali, rais alizindua mradi wa usambazaji wa stima  katika eneo la Kesogon ambao utahudumia nyumba 6,000.

Serikali, alisema, imetenga Sh330 milioni kwa eneo bunge kwa ajili ya mpango huo.

Wakati uo huo, Ruto alisema wametoa Sh1 bilioni kwa New KCC ili kununua maziwa kutoka kwa wakulima.

Alisema kuanzia mwezi ujao, wakulima watachukua Sh50 kwa kila lita ya maziwa itakayotolewa.


RADIO JAMBO FREQUENCIES

Kisumu 100.1 | Mombasa 92.3 | Nakuru 96.9 | Eldoret 99.5 | Nyeri 99.3 | Nyahururu 97.3 | Webuye 95.3 | Meru 92.7 | Kitui 104.9 | Kibwezi 104.7 | Voi 105.7 | Malindi 98.1 | Lamu 104.7 | Narok 97.3 | Kapenguria 99.7 | Kisii 89.3 | Garissa 104.3 | Maralal 97.3 | Lodwar 92.7


logo© Radio Jambo 2024. All rights reserved