Afisa wa KDF auawa kwa kushambuliwa na jiwe Kasarani

Polisi siku ya walisema kuwa wamefungua uchunguzi wa mauaji kuhusu kifo cha mawanajeswhi huyo.

Muhtasari

• Maafisa wa uchunguzi pia walizuru eneo la tukio na kuhoji wafanyakazi katika klabu hiyo ikiwa ni sehemu ya jitihada za kuwatafuta washukiwa.

crime scene 1
crime scene 1

Mwanajeshi mmoja alifariki baada ya kupigwa na jiwe kichwani katika ugomvi nje ya baa moja eneo la Mirema huko Kasarani, Nairobi.

Kelvin Ndung'u wa Moi Airbase alifariki alipokuwa akipokea matibabu katika Hospitali ya Defence Memorial Mbagathi mnamo siku ya Jumanne, Septemba 3.

Hii ilikuwa siku tatu baada ya kuhamishwa kutoka hospitali moja eneo la Kasarani ambako alikuwa amekimbizwa awali.

Ndung'u alipatikana akiwa amepoteza fahamu karibu na kilabu hicho na kuzungukwa na waendesha bodaboda dakika chache baada ya kugongwa.

Wahudumu wa bodaboda waliambia polisi Ndung'u alikuwa kwenye klabu hiyo na marafiki zake mnamo Agosti 31 wakati ugomvi ulipozuka usiku wa manane.

Walitoka nje na mmoja wa “marafiki” hao akampiga Ndung’u kichwani kwa jiwe lililomwacha amepoteza fahamu kwenye mtaro.

Mshambuliaji na marafiki zake walitoroka eneo la tukio na kumuacha akielekea kufa.

Polisi waliofika eneo la tukio dakika chache baadaye walimkimbiza katika Hospitali ya Jesse Kay eneo la Lumumba ambapo marehemu alitambuliwa kama mwanajeshi wa KDF na baadaye kuhamishiwa katika Hospitali ya Defence Forces Memorial ambako alifariki.

Polisi siku ya Jumatano walisema kuwa wamefungua uchunguzi wa mauaji kuhusu kifo cha mawanajeswhi huyo.

Wenzake waliripoti kuwa aliaga dunia kutokana na majeraha hayo alipokuwa akitibiwa.

Maafisa wa uchunguzi pia walizuru eneo la tukio na kuhoji wafanyakazi katika klabu hiyo ikiwa ni sehemu ya jitihada za kuwatafuta washukiwa.

Polisi walisema pia wanakagua kamera za usalama katika eneo hilo kama sehemu ya uchunguzi wa tukio hilo. Hakuna mtu aliyekamatwa lakini polisi walisema wanafuata miongozo.