•Msaidizi wa Bobi Wine aliibua madai kwamba kiongozi huyo wa upinzani alijeruhiwa mguuni katika makabiliano na polisi aliyevalia sare.
•"Alipelekwa katika Kituo cha Matibabu cha Najaeem huko Bulindo kwa huduma ya kwanza. Polisi watachunguza," Polisi walisema.
Jeshi la Polisi la Uganda, mnamo Jumanne jioni, lilionekana kuzua shaka kuhusu madai ya kupigwa risasi kwa mwimbaji mkongwe na mwanasiasa wa upinzani Kyagulanyi Robert Ssentamu almaarufu Bobi Wine.
Msaidizi wa Bobi Wine, Najja Ssenyonj, mapema Jumanne jioni aliibua madai kwamba kiongozi huyo wa upinzani nchini Uganda alijeruhiwa mguuni katika makabiliano na polisi aliyevalia sare.
Katika taarifa iliyosambazwa kwa umma, Jeshi la Polisi la Uganda hata hivyo lilitofautiana na madai hayo yakiashiria kwamba mwimbaji huyo wa zamani alijeruhiwa baada ya kujikwaa wakati akiingia kwenye gari lake. Haya ni kwa mujibu wa taarifa zilizotolewa na polisi waliokuwepo wakati wa mzozo kati ya Bobi Wine na maafisa hao.
“Leo tarehe 03 Septemba 2024, Mhe. Kyagulanyi Robert alialikwa na Bw. George Musisi (Wakili), kwa sherehe ya shukrani huko Bulindo, Manispaa ya Kiira, Wilaya ya Wakiso. Mhe. Kyagulanyi alishiriki katika sherehe hiyo, ambayo ilihitimishwa kwa amani,” taarifa ya polisi wa Uganda ilisomeka.
“Wakati Mhe. Kyagulanyi aliondoka ukumbini, yeye na timu yake wakatoka nje ya magari yao na kuanza msafara wa kuelekea Bulindo mjini; hata hivyo, polisi walishauri dhidi yake.
Licha ya mwongozo wao, alisisitiza kuendelea na kufunga barabara na hivyo kusababisha polisi kuingilia kati kuzuia msafara huo. Wakati wa ugomvi uliofuata, inadaiwa alipata majeraha.
Askari polisi waliopo eneo hilo wanadai alijikwaa wakati akiingia kwenye gari lake na kusababisha jeraha, ambapo Mhe. Kyagulanyi na timu yake wanadai kuwa alipigwa risasi,” taarifa hiyo ilisomeka zaidi.
Idara ya polisi ilisema kuwa uchunguzi unaendelea ili kubaini ukweli kuhusu madai mawili tofauti yaliyotolewa na pande zote mbili.
"Alipelekwa katika Kituo cha Matibabu cha Najaeem huko Bulindo kwa huduma ya kwanza. Polisi watachunguza madai ya kupigwa risasi na matukio yoyote yanayohusiana nayo,” polisi walisema.
Taarifa ya polisi ilitofautiana na taarifa ya msaidizi wa Bobi Wine iliyodai kuwa kiongozi wa upinzani Bobi Wine alijeruhiwa mguuni katika makabiliano na polisi aliyevalia sare na alipelekwa kwa matibabu katika Hospitali ya Nsambya katika mji mkuu, Kampala.