Kaimu IG Masengeli akiuka agizo la kufika mahakamani tena

Hii ni mara ya tatu kwa Kaimu IG kukosa kujiwasilisha mbele ya mahakama kama alivyoagizwa.

Muhtasari

• Mahakama ilitaka aje kueleza kwa nini hapaswi kutuhumiwa na mahakama kuhusu kesi ya watu waliotoweka.

Kaimu Inspekta Jenerali wa Polisi Gilbert Masengeli. Picha: NPS/X
Kaimu Inspekta Jenerali wa Polisi Gilbert Masengeli. Picha: NPS/X

Kaimu Inspekta Jenerali wa Polisi Robert Masengeli amekosa kufika mahakamani kama ilivyotarajiwa kuhusiana na tuhuma za kukiuka amri za mahakama.

Mahakama iliambiwa kuwa Kaimu IG alikuwa hayupo akihudhuria warsha mjini Mombasa na hivyo hangeweza kuhudhuria korti.

Hii ni mara ya tatu kwa Kaimu IG kukosa kujiwasilisha mbele ya mahakama kama alivyoagizwa.

Mahakama ilitaka aje kueleza kwa nini hapaswi kutuhumiwa na mahakama kuhusu kesi ya watu waliotoweka.

Siku ya Jumanne, Jaji Lawrence Mugambi alisema angempa nafasi ya kujitetea kabla ya kutaja madhara ya kutotii maagizo ya mahakama.

"Mahakama inapaswa kusisitiza mamlaka yake juu ya kudumisha utawala wa sheria ambapo uasi wa makusudi wa maagizo yake umedhihirika. Hata hivyo hii ni mamlaka ambayo lazima itumike kwa uangalifu mkubwa," alisema Mugambi.

Mahakama ilikuwa ikimtarajia Masengeli kufika kortini Jumanne kuhojiwa kuhusu kutoweka kwa watu watatu eneo la Kitengela wiki mbili zilizopita. Lakini hakufanya hivyo.

Jaji alifahamishwa na mawakili wake kwamba yuko nje ya ofisi kwa majukumu rasmi.

Lakini LSK kupitia kwa rais wao Faith Odhiambo ilisema IG bado ana dharau baada ya kuitwa kufika kortini.

"Hawaonyeshi nia ya kuheshimu maagizo ya mahakama. Majukumu rasmi yanayodaiwa sio muhimu kuliko maisha ya binadamu," alisema.

Odhiambo alidai kuwa IG hajawasilisha ushahidi wowote kuonyesha kuwa IG yuko nje ya mji.

Walitaka hati ya kukamatwa itolewe dhidi yake.

"Ameidharau mahakama kwa kupuuza hoja ya Haki. Familia za walalamishi hazijawaona au kusikia chochote kinachohusu jamaa zao, wamefadhaika," aliongeza.

 

Jaji Mugambi alikubaliana na LSK kwamba kila mtu ana haki ya kufurahia haki na uhuru wa kimsingi. Alisema ni jukumu la serikali kulinda haki na uhuru wa kimsingi katika Sheria ya Haki.

 

"Hii ni nchi inayoongozwa kwa sheria sio akili za watu. Mahakama ina meno na inaweza kuuma, wale wanaopuuza maagizo ya mahakama kwa makusudi lazima wawe tayari kukabiliana na matokeo yake," alisema Jaji.

Hata hivyo alimruhusu IG kujitetea kabla ya kutoa amri nyingine.