Rais William Ruto amuomboleza naibu gavana wa Lamu

Bw Ndung’u alikata roho Ijumaa Septemba 6, 2024 katika Hospitali ya Nairobi alikokuwa akipokea matibabu.

Muhtasari

•Rais Ruto alimtaja marehemu kama kiongozi mwenye maendeleo ambaye alifanya kazi bila kuchoka kwa ajili ya watu wa Lamu.

•Gavana wa Lamu Issa Timamy alifichua kuwa naibu wake alipoteza maisha mwendo wa saa kumi na mbili unusu jioni ya Ijumaa.

Marehemu Raphael Munyua Ndung'u
Image: HISANI

Rais William Ruto ameungana na wananchi wa kaunti ya Lamu kuomboleza kifo cha naibu gavana wao Raphael Munyua Ndung’u.

Bw Ndung’u alikata roho mnamo Ijumaa Septemba 6, 2024 katika Hospitali ya Nairobi alikokuwa akipokea matibabu baada ya kuugua.

Huku akimuomboleza, rais Ruto alimtaja marehemu kama kiongozi mwenye maendeleo ambaye alifanya kazi bila kuchoka kwa ajili ya watu wa Lamu.

"Nimesikitishwa na taarifa za kuaga kwa Naibu Gavana wa Kaunti ya Lamu Raphael Munyua Ndung'u," Rais Ruto alisema.

Rais pia alituma risala zake za rambirambi kwa familia ya marehemu mwanasiasa huyo na watu wote wa kaunti ya Lamu kwa msiba wao.

“Alikuwa kiongozi mwenye maendeleo ambaye alifanya kazi bila kuchoka kwa manufaa makubwa ya watu wa Lamu. Upendo na maombi yetu kwa familia, marafiki na watu wa Kaunti ya Lamu wakati huu wa huzuni. Pumzika kwa Amani,” aliongeza.

Gavana wa Lamu Issa Timamy alifichua kuwa naibu wake alipoteza maisha mwendo wa saa kumi na mbili unusu jioni ya Ijumaa.

Katika salamu zake za rambirambi, mkuu huyo wa kaunti alimtaja marehemu kuwa ni zaidi ya makamu wake.

“Alikuwa mfanyakazi mwenza, rafiki wa karibu, kaka, mtumishi aliyejitolea wa watu wa Lamu. Kujitolea kwake bila kuyumba kwa maendeleo na ustawi wa kaunti yetu kulionekana katika kila kazi aliyoifanya, na shauku yake ya kuinua maisha ya watu wetu haikuwa na kifani,” Timamy alisema.

Gavana huyo aliendelea kuwapa pole familia ya Munyua na kuwataka wenyeji wa Lamu kumuenzi marehemu kwa kuendelea na kile alichokiamini.