Wanafunzi wa vyuo kikuu wakaribisha timu ya Ogamba, wasitisha mgomo

Sehemu ya viongozi wa wanafunzi wamekaribisha tangazo la serikali la kuunda kamati ya kukagua mtindo Mpya wa Ufadhili wa Vyuo Vikuu.

Muhtasari

•Waziri wa Elimu Julius Ogamba alitangaza Jumapili kwamba serikali wiki hii itaunda kamati mbili za kukagua mtindo huo.

•Viongozi hao walidai kuwa wahuni walikuwa wamehamasishwa kupenya maandamano siku ya Jumatatu.

Sehemu ya viongozi wa vyuo vikuu wakihutubia wanahabari Septemba 8, 2024
Sehemu ya viongozi wa vyuo vikuu wakihutubia wanahabari Septemba 8, 2024

Sehemu ya wanafunzi wa vyuo vikuu wamekaribisha tangazo la serikali la kuunda kamati ya kukagua mtindo Mpya wa Ufadhili wa Vyuo Vikuu.

Waziri wa Elimu Julius Ogamba alitangaza Jumapili kwamba serikali wiki hii itaunda kamati mbili za kukagua mtindo huo huku kukiwa na vitisho vya mgomo kutoka kwa wanafunzi.

Sehemu ya viongozi wa wanafunzi wakiongozwa na Katibu Mkuu wa Chama cha Wanafunzi wa Chuo Kikuu cha Nairobi Ramesh Saxena walisema wamesitisha maandamano yaliyopangwa Jumatatu ili kutoa nafasi kwa mazungumzo.

“Tunaamini maandamano ya mitaani si njia bora kwa sasa isipokuwa hatuna njia nyingine, wandugu tunaona mwanga mwisho wa handaki... tunaungana na viongozi wetu wa wanafunzi waliohutubia vyombo vya habari jana (Jumamosi) kusitisha shughuli ya kesho na kurudi kwenye meza ya majadiliano kuhusu suala hili," walisema katika taarifa ya pamoja.

Wengine waliokuwepo kwenye kikao na wanahabari jijini Nairobi ni Zadock Nyakwaka (KU), Henry Odiwuor (Chuo Kikuu cha Zetec), Austin Onyango (Chuo Kikuu cha KCA), Adrian Oluoch (Chuo Kikuu cha Chuka), Dkt Ojwang (UoN), na wengine.

Viongozi hao wa wanafunzi waliojumuisha maafisa ambao hawakuchaguliwa kutoka vyuo vikuu walidai kuwa wahuni walikuwa wamehamasishwa kupenya maandamano siku ya Jumatatu.

"Tunaungana na viongozi wetu wa wanafunzi waliozungumza na vyombo vya habari jana kusitisha shughuli ya kesho na kurejea kwenye meza ya majadiliano juu ya jambo hili. Tubaki salama, na watulivu tunapofuatilia suala hili kwa ufumbuzi wa amani na ushindi wa kishindo kwa wote. wandugu,” walisema.

Viongozi hao ambao walisema wanafahamu mipango ya Serikali ya kuunda kamati ya kupitia mtindo huo walisema ni lazima hadidu za rejea za kamati hiyo ziharakishwe ili mchakato huo uanze haraka iwezekanavyo.

“Tunaomba nia hii njema iharakishwe ili tiba za muda mfupi ziangaliwe huku dhamira ikiwekwa kwa ajili ya kutatua tatizo hili kwa muda mrefu,” walisema.

"Kama viongozi, tunaunga mkono mbinu hiyo mpya lakini tunatoa wito kwa serikali kuwezesha kuandaa ratiba madhubuti na TOR kwa kazi za kamati."

Wandugu hawatakubali kuridhika tena, turekebishe na tuendelee kama nchi, walisema.

Wakati huo huo, wanafunzi hao waliitaka serikali kwa kushauriana na uongozi wa vyuo vikuu kupunguza kile walichokiita gharama kubwa za malazi na kushughulikia makataa ya karo.