Kaimu IG, Masengeli ahukumiwa miezi sita jela kwa kudharau mahakama

Amepatikana na makosa ya kudharau mahakama mara saba

Muhtasari

• Masengeli anatuhumiwa kwa kosa la kutoheshimu mahakama kufika mbele yake kujibu maswali ya Wakenya watatu kutoweka Kitengela mikononi mwa Polisi.

• Masengeli ataanza kutumikia kifungo chake baada ya siku saba ya kusomwa hukumu yake

Kaimu Inspekta Jenerali wa Polisi Gilbert Masengeli.
Kaimu Inspekta Jenerali wa Polisi Gilbert Masengeli.
Image: Picha: NPS/X

Kaimu Inspekta Jeneralii wa polisi Gilbert Masengeli amehukumiwa kifungo cha miezi sita jela. 

Akisomewa hukumu na jaji Lawrence Mugambi wa mahakama ya Milimani siku ya Ijumaa alisema kuwa Masengeli alijaribu kumtuma naibu wake katika hatua za mwisho ila mahakama ilipuuzilia mbali hatua hiyo na kumtaka mwenywe kujiwajibisha mahakamani.

Jaji alisikitika kuwa Masengeli alichagua kudhihaki mahakama na kuelekea Mombasa kwa mkutano wa maafisa wakuu wa usalama.

Masengeli amehukumiwa kwa kosa la kukaidi amri ya korti ambapo alitakiwa kufika mbele ya jaji Mugambi wa mahakama ya Milimani kuelezea hatma ya watu watatu wakiwemo ndugu wawili waliotoweka eneo la Kitengela baada ya kutekwa na watu wanaoaminika kuwa maafisa wa polisi mnamo tarehe 19 Juni mwaka huu.

Wanaodaiwa kupotea wanakisiwa kuwa kati ya waandalizi wakuu wa maandamano ya kupinga mswada wa fedha wa mwaka 2024/2025 ambao ulitupiliwa mbali na rais William Ruto.

Masengeli ambaye anashikilia nafasi ya Inspekta jenerali wa polisi kikaimu, alikosa kufika mbele ya mahakama mara saba kueleza walipo wakenya waliotoweka katika kesi iliyowasilishwa mahakamni na chama cha wanasheria nchini LSK.

Mahakama imempata Masengeli na kosa la kukaidi korti na kumtaka waziri wa uslama wa ndani Prof Kithure Kindiki kuhakikisha Masengeli anatumikia kifungo chake kikamilifu.

Jaji Mugambi ameamuru Masengeli kujisalamisha kwa kamishna jenerali wa magereza kuanza kuhudumia kifungo chake la sivyo Prof Kindiki ameombwa na mahakama kushirikiana na kamishna jenerali wa magereza kuhakikisha Masengeli hakwepi kifungo chake.

Mawakili wa Masengeli walieleza mahakama kuwa mteja wao alikosa kujitokeza mahakamani kwani alikuwa anaongoza mkutano wa wakuu wa polisi wa kaunti katika hafla iliyofanyika kaunti ya pwani. 

Masengeli ataanza kifungo chake cha miezi sita jela baada ya siku saba ya kusomewa hukumu.

Jaji Mugambi ameamuru Masengeli kujisalamisha 

Hata hivyo amepewa nafasi ya kujiwasilisha tena mahakamani.