Kenya mshirika mkuu wa Tamasha za Bürgerfest

Kwa mara ya kwanza nchi ya nje ya Ulaya inashirikiana na Ujerumani kwa Tamasha za hadhi ya juu

Muhtasari

• Rais Ruto yupo nchini Ujerumani kwa ziara ya kikazi na kutia saini mikataba ya ushirikiano baina ya Kenya na mwenyeji wake.

• Sherehe za Bürgerfest zitaandaliwa Jumamosi 14 na Kenya ni mshirika mkuu wa tamasha hizo.

akiabiri ndege
Rais William Ruto akiabiri ndege
Image: PCS

Taifa la Kenya litakuwa nchi ya kwanza nje ya bara la Ulaya kuwa mshirika mkuu wa tamasha za kila mwaka za wananchi nchini Ujerumani.

Tamasha hizo zenye hadhi ya juu zaidi Ujerumani zinazojulikana kwa jina Bürgerfest zimepewa  kauli mbiu ya  "Pamoja - Stronger together" .  Sherehe za Bürgerfest zitafanyika Jumamosi.

Tamasha hizo zinalenga kuonyesha utajiri wa utamaduni wa Kenya na jamii ya Ujerumani na kubadilishana tamaduni hizo.

Akizungumza kabla ya kufanyika kwa Tamasha hilo litakalohudhuriwa na rais William Ruto, katibu katika wizara ya mambo ya kigeni Korir Song'oei alisema, "Kenya inaitazama Ujerumani kama mshirika wa lazima katika hatua za maendeleo, ukuaji na utulivu."

Vile vile Sing'oei alitaja ushirikiano huo wa Kenya na Ujerumani kupitia tamasha hilo la Jumamosi 15 ni hatua kubwa katika kuendeleza uhusiano mwema baina ya nchi hizi mbili.

Rais Ruto alisafiri kuelekea Ujerumani usiku wa Alhamisi ambako ni ziara kikazi nchini Ujerumani.

Mbali na kuwa mgeni wa Bürgefest, rais pia atatia sahihi makubaliano ya kibiashara baina ya Kenya na Ujerumani.

Ziara ya rais inalenga kutafuta nafasi za ajira kwa vijana wa Kenya kufanya kazi Ujerumani, kupata nafasi za elimu na mafunzo ya kazi pamoja na kutia mkataba wa maelewano ya kina ya kusafirisha vijana wa kazi.

Rais pia atafanya kikao na rais wa Ujerumani Frank-Walter Steinmeier na chansela Olaf Scholz.