Jaji Mkuu Martha Koome adai kurejeshwa kwa walinzi wa jaji aliyemhukumu Masengeli

Koome ameibua wasiwasi kuhusu madai hayo na kusema kuwa suala kama hilo ni mojawapo ya yanayomkosesha usingizi usiku.

Muhtasari

•Walinzi wa Mugambi wanadaiwa kuondolewa baada ya kumhukumu Kaimu Inspekta Jenerali wa Polisi Gilbert Masengeli kifungo cha miezi sita jela.

Jaji Mkuu Martha Koome
Image: MAKTABA

Jaji Mkuu Martha Koome ameitaka Huduma ya Kitaifa kwa Polisi kurejesha mara moja maafisa wa usalama wa Jaji Lawrence Mugambi.

Walinzi wa hakimu huyo wanadaiwa kuondolewa baada ya kumhukumu Kaimu Inspekta Jenerali wa Polisi Gilbert Masengeli kifungo cha miezi sita jela.

Hakimu Mkuu mnamo Jumatatu aliibua wasiwasi kuhusu madai hayo na kusema kuwa suala kama hilo ni mojawapo ya mengine mengi yanayomkosesha usingizi usiku.

Katika kikao na wanahabari katika majengo ya Mahakama ya Juu, Koome ambaye ni Mwenyekiti wa Tume ya Huduma za Mahakama (JSC) alikashifu vikali kitendo hicho cha vitisho na kuwahakikishia Wakenya wataendelea kusimama kidete hata wakabiliane na nini.

"Ni muhimu kukumbuka kuwa uhuru wa mahakama si haki ya Majaji; ni msingi wa haki kwa raia wote. Majaji lazima wawe huru kufanya maamuzi kwa kuzingatia sheria pekee, bila kuogopa kuadhibiwa au kuingiliwa," alisema Koome.

"Uingiliaji wowote wa uhuru huu unaweka jamii yetu katika hatari ya kutumbukia katika uvunjaji sheria, ambapo kunaweza kuchukua nafasi ya haki, na haki inapotoshwa na vitisho," aliongeza.

Kauli hiyo ya mahakama inafuatia baada ya Masengeli kutiwa hatiani na kuhukumiwa na Hakimu kwa kosa la kuidharau mahakama.

Jaji Mugambi mnamo Ijumaa aliamuru ajiwasilishe kwa kamishna mkuu wa magereza.

"Ikitokea, hatajiwasilisha mwenyewe Waziri wa Mambo ya Ndani lazima achukue hatua zote kuhakikisha anafungwa gerezani ili kutumikia kifungo," alisema Jaji.

Mugambi hata hivyo alisema Masengeli huenda akakwepa kutumikia kifungo hicho iwapo atafikishwa mahakamani ndani ya siku saba zijazo.