IPOA yachunguza kutolewa kwa walinzi wa hakimu Lawrence Mugambi

Baada ya JSC kulalamikia kutolewa kwa walinzi wa jaji aliye kazini kikamilifu.

Muhtasari

• JSC ililalamikia hatua ya kuondolewa kwa walinzi wa hakimu Lawrence Mugambi siku chache baada ya kumhukumu kaimu IG kifungo cha miezi 6 jela.

• IPOA inasema tayari uchunguzi umeanzishwa kwa madai ya kuondolewa walinzi wa hakimu Mugambi.

Mwenyekiti wa IPOA
ANNE MAKORI Mwenyekiti wa IPOA
Image: HISANI

Mamlaka ya kuangalia utendakazi wa maafisa wa polisi IPOA imetoa taarifa kuwa imeanzisha uchunguzi kufuatia madai ya kuondolewa kwa walinzi wa hakimu Lawrence Mugambi.

Tume ya huduma za mahakama ikiongozwa na rais wake jaji Martha Koome siku ya Jumapaili ililalamikia hatua ambapo walinzi wa hakimu Mugambi waliondolewa baada ya kumhukumu kaimu inspekta jenerali wa Gilbert Masengeli kifungo cha miezi sita jela kwa kudharau mahakama.

IPOA imesema kwamba imeanzisha uchunguzi wa madai ya kuondolewa kwa polisi waliokuwa wakimwekea hakimu Mugambi ulinzi kwa mujibu wa kifungu cha 6 cha sheria ya mamlaka huru ya uangalizi wa polisi.

Mamlaka hiyo imesema kuwa baada ya uchunguzi kufanywa, itatoa mapendekezo ikiwemo kufungua mashtaka kwa washukiwa watakaopatikana na uvujaji wa sheria.

Aidha, IPOA imeonya kuwa hatua ya kaimu inspekta jenerali wa polisi kudharau maagizo ya kaorti inakiuka kifungo cha 244 cha katiba.

IPOA imeendelea kusema kuwa huo ni mfano hatari ambao utahimiza ikiukaji wa sheria.

Hata hivyo, ofisi ya inspekta jenerali wa polisi awali ilijibu madai ya tume ya huduma za mahakama JSC ikisema kuwa walinzi wa hakimu Mugambi hawakuondolewa makusudi bali walitakiwa kushiriki mafunzo zaidi ya ulinzi.

Vile vile, kaimu IG Masengeli alisema kuwa NPS ina wajibu wa kutoa ulinzi kwa rais, naibu rais na marais wastaafu pekee.

Walinzi wa hakimu Mugambi waliondolewa siku chache baada ya kumhukumu kaimu IG Gilbert Masengeli kifungo cha miezi sita jela.