Douglas Kanja aapishwa kuwa Inspekta Jenerali wa polisi

Ni mwanzo wa uongozi wake kama Inspekta Jenerali wa tano wa polisi chini ya Katiba ya 2010.

Muhtasari

•Kanja anachukua nafasi ya Japhet Koome ambaye alijiuzulu mnamo Julai baada ya wimbi la maandamano ya Gen Z.

Inspekta Jenerali wa Polisi Douglas Kanja akila kiapo katika majengo ya Mahakama ya Juu mnamo Septemba 19, 2024.
Inspekta Jenerali wa Polisi Douglas Kanja akila kiapo katika majengo ya Mahakama ya Juu mnamo Septemba 19, 2024.
Image: HISANI

Inspekta Jenerali wa Huduma ya Kitaifa kwa Polisi Douglas Kanja mnamo Alhamisi mchana alikula kiapo katika majengo ya Mahakama ya Juu.

Huu sasa unaashiria mwanzo wa uongozi wake kama Inspekta Jenerali wa tano wa polisi chini ya Katiba ya 2010.

Anachukua nafasi ya Japhet Koome ambaye alijiuzulu mnamo Julai baada ya wimbi la maandamano ya Gen Z kuhusu Sheria ya Fedha ya 2024.

Kanja alijumuika na familia yake wakati wa hafla ya kuapishwa iliyoongozwa na Jaji Mkuu Martha Koome.

Aliapishwa saa chache baada ya Rais William Ruto kuchapisha jina lake kwenye gazeti la serikali kushika wadhifa huo.

Hii inafuatia kuidhinishwa na Bunge la Kitaifa siku ya Jumatano. Hapo awali alikuwa ameidhinishwa na Seneti baada ya kukaguliwa.

"Mimi William Ruto nimemteua Douglas Kanja Kirocho kuwa Inspekta Jenerali wa Huduma ya Kitaifa ya Polisi kwa muhula wa miaka 4," notisi ya gazeti iliyofikia Radio Jambo ilisema.

Kanja ndiye aliyekuwa Naibu Inspekta Jenerali wa Polisi wa Kenya.

Awali alihudumu kama Kamanda Mkuu wa kitengo cha GSU.