Masengeli aomba radhi mahakama, asema hatua zake hazikuwa za makusudi

Masengeli alisimama na kueleza kuwa kitendo chake si cha makusudi.

Muhtasari

•Masengeli mnamo Ijumaa mchana ameiomba radhi mahakama kwa matukio yaliyotokea hadi kutiwa hatiani na kuhukumiwa kwake.

•"Naomba kwamba mahakama hii ikubali ombi langu la msamaha na iondoe hatia na hukumu," Masengeli alisema.

akiwa na Wakili wake Cecil Miller mahakamani Septemba 20. 2024
Naibu IG Gilbert Masengeli akiwa na Wakili wake Cecil Miller mahakamani Septemba 20. 2024
Image: EZEKIEL AMINGA

Naibu Inspekta Jenerali wa Polisi Gilbert Masengeli mnamo Ijumaa mchana ameiomba radhi mahakama na idara ya mahakama kwa matukio yaliyotokea hadi kutiwa hatiani na kuhukumiwa kwake.

Masengeli alisimama na kueleza kuwa kitendo chake si cha makusudi.

Alimwambia Jaji Lawrence Mugambi kwamba alihusika katika masuala ya usalama wa kitaifa ambayo yalihitaji umakini wake wa pekee katika eneo la kaskazini mwa Kenya.

“Nakuheshimu wewe na mahakama zetu zote kwa kazi nzuri unayoifanya ya kuzingatia utawala wa sheria, mimi nikiwa askari polisi ni wajibu wangu kusimamia amri za mahakama na kuhakikisha amri za mahakama zinatii,” alisema Masengeli.

"Naomba kwamba mahakama hii ikubali ombi langu la msamaha na iondoe hatia na hukumu," Masengeli alisema.

Aliambia mahakama kuwa juhudi zilifanywa kuhusiana na kutoweka kwa raia watatu wa Kitengela na uchunguzi bado unaendelea.

Masengeli anashikilia kuwa watatu hao wa Kitengela hawakuwahi kufungwa lakini Ijumaa asubuhi amefahamu kutoka kwa wakili Nelson Havi kwamba wamepatikana.

Havi ametoa kauli hiyo mahakamani hapo mapema leo asubuhi alipokuwa akiwasilisha shauri hilo.

"Mimi siko juu ya sheria, nimetii amri za mahakama," Masengeli alisema wakati akitetea haki yake ya kuendelea kushika wadhifa wa umma.