Mwanaharakati na ndungu wawili waliotekwa Kitengela wapatikana wakiwa hai

Jamil Longton na kakake Aslam walitupwa kwenye mpaka wa Gachie wa Kiambu na Nairobi na watekaji wao.

Muhtasari

• Kuachiliwa kwa watatu hao kulijiri saa chache baada ya Inspekta Jenerali mpya wa Polisi Douglas Kanja kushikilia kuwa watatu hao hawakuwa mikoni mwa polisi.

Mwanaharakati Bob Njagi na ndungu wawili Jamil na Aslay Longton, waliokuwa wametekwa nyara Kitengela.
Mwanaharakati Bob Njagi na ndungu wawili Jamil na Aslay Longton, waliokuwa wametekwa nyara Kitengela.

Ndugu wawili na mwanaharakati waliotoweka mnamo Agosti 19, 2024 kufuatia maandamano ya kuipinga serikali huko Kitengela, wamepatikana wakiwa hai katika Kaunti ya Kiambu.

Mwanaharakati Bob Njagi alipatikana akiwa hai katika eneo la Tigoni, Kaunti ya Kiambu. Rais wa Chama cha Wanasheria LSK Faith Odhiambo alisema kwamba mratibu wa Free Kenya Movement, Bob Njagi, alipatikana akiwa hai. 

Alisema Njagi alijiwasilisha katika kituo cha polisi cha Tigoni baada ya kutupwa na watekaji nyara eneo hilo. "Mnamo saa saba usiku Bob Njagi alifanikiwa kutafuta njia hadi kituo cha polisi cha Tigoni na kupata usaidizi. Yuko hai," Odhiambo alisema. 

Rais wa huyo wa LSK alithibitisha kuwa mwanaharakati huyo alikuwa amemtumia ujumbe akithibitisha kuwa yuko salama. 

"Ujumbe kutoka kwa Bob na familia, 'Kwa familia, marafiki na kila Mkenya ambaye ameendelea kuniombea, napenda kuthibitisha kuwa mimi ni mzima na pamoja na familia yangu. Sasa ni wakati wa kutuliza kelele, kushukuru kwa maisha. na kwa kila mtu kutafakari kwa nini Kenya ni muhimu," Njagi alisema, kulingana na rais wa LSK.

Wakati huo huo rais wa LSK alisema ndungu wawili Jamil na Aslay Longton walipatikana wametupwa eneo la Gachie, Kaunti ya Kiambu.

Jamil Longton na kakake Aslam walitupwa kwenye mpaka wa Gachie wa Kiambu na Nairobi na watekaji wao.

Odhiambo alisema alisema kuachiliwa kwa watatu hao kumetokana na kesi waliowasilisha mahakamani na shinikizo za mashirika ya kijamii.

Kuachiliwa kwa watatu hao kulijiri saa chache baada ya Inspekta Jenerali mpya wa Polisi Douglas Kanja kushikilia kuwa watatu hao hawakuwa mikoni mwa polisi.