logo

NOW ON AIR

Listen in Live

Maandalizi kabambe yafanyika usiku kucha ukumbini KICC tayari kwa kuapishwa kwa Kindiki

Awali, serikali ilichapisha katika gazeti lake rasmi ikitaarifu umma kwamba Ijumaa leo itakuwa ni sikukuu kutoa nafasi kwa ajili ya kuapishwa kwa Kindiki .

image
na MOSES SAGWEjournalist

Yanayojiri01 November 2024 - 08:19

Muhtasari


  • Watu walionekana wakipanga viti, wengine wakitandika maturubai na kupamba eneo hilo kwa rangi rasmi za kiserikali kwa ajili ya shughuli hiyo ya kiserikali.
  • Awali, serikali ilichapisha katika gazeti lake rasmi ikitaarifu umma kwamba Ijumaa leo itakuwa ni sikukuu kutoa nafasi kwa ajili ya kuapishwa kwa Kindiki 

Ukumbi wa kimataifa wa KICC ulishuhudia shughuli nyingi usiku wa Alhamisi kuamkia Ijumaa baada ya taarifa kuwekwa wazi kwamba hilo ndilo eneo atakapoapishiwa Profesa Abraham Kithure Kindiki kama naibu rais.

Ikulu ilitoa taarifa kwa umma kwamba KICC itandaa hafla ya kuapishwa kwa Kindiki kuanzia majira ya saa nne asubuhi Ijumaa, muda mfupi baada ya mahakama kuu kuondoa amri ya kuzuia kuapishwa kwake.

Katika picha na video ambazo zimeonekana na meza yetu ya habari, watu kadhaa walionekana walihaha hapa na pale kufanya maandalizi katika ukumbi huo usiku kucha, tayari kwa kuapishwa kwa Kindiki.

Watu walionekana wakipanga viti, wengine wakitandika maturubai na kupamba eneo hilo kwa rangi rasmi za kiserikali kwa ajili ya shughuli hiyo ya kiserikali.

Awali, serikali ilichapisha katika gazeti lake rasmi ikitaarifu umma kwamba Ijumaa leo itakuwa ni sikukuu kutoa nafasi kwa ajili ya kuapishwa kwa Kindiki kama naibu rais. Kindiki ambaye mpaka kuteuliwa kwake kuhudumu kama naibu rais, alikuwa anashikilia wadhifa wa waziri wa masuala ya ndani, sasa ameachia kiti hicho kwa waziri mwenye mamlaka makuu Musalia Mudavadi.

Mudavadi aliteuliwa na Ruto kuhudumu kama waziri wa masuala ya ndani kikaimu.

Kindiki aliteuliwa na Ruto kama naibu wake takribani wiki mbili zilizopita baada ya seneti kumbandua Rigathi Gachagua kama naibu rais kwa kupigia kura hoja 11 za mashtaka dhidi yake, kama yalivyowasilishwa na mbunge wa Kibwezi Magharibi, Mwengi Mutuse.

Hata hivyo, Kindiki hakuweza kuapishwa baada ya mawakili wa Rigathi Gachagua kuelekea katika mahakama ya Kerugoya kaunti ya Kiriganya na kupewa amri ya kusitisha kuapishwa kwake, wakidai kwamba mteja wao hakupewa nafasi ya kujitetea kwenye seneti baada ya kuugua ghafla.


RADIO JAMBO FREQUENCIES

Kisumu 100.1 | Mombasa 92.3 | Nakuru 96.9 | Eldoret 99.5 | Nyeri 99.3 | Nyahururu 97.3 | Webuye 95.3 | Meru 92.7 | Kitui 104.9 | Kibwezi 104.7 | Voi 105.7 | Malindi 98.1 | Lamu 104.7 | Narok 97.3 | Kapenguria 99.7 | Kisii 89.3 | Garissa 104.3 | Maralal 97.3 | Lodwar 92.7


logo© Radio Jambo 2024. All rights reserved