logo

NOW ON AIR

Listen in Live

Ndoa ya kisiasa kati ya Ruto na Gachagua yafika mwisho huku Kindiki akiapishwa kama DP

Katika kipindi chote cha kujadiliwa kwa mswada wa kumbandua Gachagua ofisini, bosi wake William Ruto alisalia katika kimya kikuu.

image
na MOSES SAGWEjournalist

Yanayojiri01 November 2024 - 09:59

Muhtasari


  • Alhamisi Oktoba 31, mahakama kuu ya Nairobi ikiongozwa na jopo la majaji 3 walibatilisha agizo hilo na kutoa fursa kwa Kindiki kuapishwa.
  • Kindiki ameapishwa Novemba 1 katika ukumbi wa kimataifa wa KICC katika hafla iliyohudhuriwa na makumi ya Wakenya.

Ndoa ya kisiasa baina ya Rigathi Gachagua na Rais William Ruto imefika mwisho hatimaye leo hii Novemba mosi 2024 kufuatia kuapishwa kwa Kithure Kindiki kama naibu rais mpya.

‘Ndoa’ hii ilianza mwaka 2022 Septemba 13 baada ya Gachagua na Ruto kuapishwa kama naibu rais na rais mtawalia, lakini miaka miwili baadae, wawili hao wamegeuka kuwa mahasimu wa kisiasa wasioweza kuonana jicho kwa jicho.

Ilikuaje?

Ruto na Gachagua walikuwa na uhusiano mzuri mpaka mapema mwaka huu wakati rais alikaribisha chama cha upinzani ODM serikali kuunda serikali jumuishi jambo ambalo lilionekana kutomridhisha Gachagua.

Baadae, Gachagua alituhumiwa kwa kutoa matamshi yasiyofaa dhidi ya serikali anayoihudumia na viongozi serikali wakaanzisha mchakato wa kumbandua.

Baada ya kisia kisia za muda, hatimaye mswada wa kumbandua Gachagua uliwasilishwa bungeni na mbunge wa Kibwezi Magharibi, Mwengi Mutuse, hata licha ya wandani wa rais kukanusha kuwepo kwa mswada huo awali.

Katika kipindi chote cha kujadiliwa kwa mswada wa kumbandua Gachagua ofisini, bosi wake William Ruto alisalia katika kimya kikuu.

Na Gachagua alitimuliwa ofisini takribani wiki mbili zilizopita baada ya seneti kupiga kura ya kuidhinisha hoja zote 11 zilizowasilishwa kama mashtaka dhidi yake.

Kuapishwa kwa Kindiki kama naibu rais mpya kulipigwa breki baada ya mawakili kuelekea katika mahakama ya Kerugoya na kupata agizo la kuzuia kuapishwa kwake.

Alhamisi Oktoba 31, mahakama kuu ya Nairobi ikiongozwa na jopo la majaji 3 walibatilisha agizo hilo na kutoa fursa kwa Kindiki kuapishwa.

Kindiki ameapishwa Novemba 1 katika ukumbi wa kimataifa wa KICC katika hafla iliyohudhuriwa na makumi ya Wakenya.

Siku hiyo ilitangazwa kuwa sikukuu kwa ajili ya kutoa fursa kwa kuapishwa kwa msomi huyo wa kisheria ambaye awali alihudumu kama waziri wa masuala ya ndani.


RADIO JAMBO FREQUENCIES

Kisumu 100.1 | Mombasa 92.3 | Nakuru 96.9 | Eldoret 99.5 | Nyeri 99.3 | Nyahururu 97.3 | Webuye 95.3 | Meru 92.7 | Kitui 104.9 | Kibwezi 104.7 | Voi 105.7 | Malindi 98.1 | Lamu 104.7 | Narok 97.3 | Kapenguria 99.7 | Kisii 89.3 | Garissa 104.3 | Maralal 97.3 | Lodwar 92.7


logo© Radio Jambo 2024. All rights reserved