Maafisa wa ujasusi wanaochunguza kisa ambapo mwili wa mtu
asiyejulikana ulipatikana na majeraha mabaya katika eneo la Lang’ata wanasema
kuwa huenda mwathiriwa aliuwawa na mshukiwa mkuu wa mauaji ya mwanamke na
mwanawe pamoja na mpwa wake kutoka mtaani Eastleigh kaunti ya Nairobi.
Maafisa hao wamesema kupitia ukurasa wa X kuwa mkondo wa
uchunguzi umepata mwanya mkubwa wa kutambua mshukiwa aliyetupa mwili wa marehemu
uliopatikana mnamo Oktoba 31. Kwa mujibu wa DCI, mshukiwa mkuu wa mauaji ya
familia moja kutoka Eastleigh Hashim Dagane huenda alihusika na ukatili huo.
Kulingana na taarifa ya DCI kutokana na vifaa vya ushahidi
walivyokusanywa palipotupwa mwili wa marehemu, uchunguzi uliwaelekeza katika
duka la jumla la Quickmart kati kati mwa jiji la Nairobi na kubaini kuwa mwanamke
anayedaiwa kuuliwa na mwili wake kutupwa huenda ulikuwa wa mwanamke alioenekana
kwenye kanda za CCtv za duka hilo tarehe 29 Oktoba.
Uchunguzi umebaini pia mwanamke huyo alielekea katika sehemu
ya makazi kwenye mtaa Lavington ambapo pia kamera za siri zilimnasa akiingia
nyumbani huko.
Polisi wanaamini kuwa mwanamke huyo alikuwa pamoja na Hashim katika nyumba
hiyo.
Baada ya kukagua kamera za CCtv, polisi waligundua kuwa siku
iliyofuata Hashim alitoka na mifuko miwili mikubwa inayoshukiwa kuwa mabaki ya
mwili ya marehemu aliyotupa eneo la Lang’ata.
Kufuatana na uchunguzi huo, polisi wanaamini kuwa mwili wa
mwanamke uliopatikana ni wa Deka Abdinoor Gorone aliyeripotiwa kupotea katika kituo
cha polisi cha California tarehe 24 Oktoba.
Hata hivyo polisi wanamtafuta mmiliki wa nyumba inayodaiwa
kuwa Hashim alitekeleza unyama wake katika eneo la Lavington ambaye inaaminika
kuwa baada ya kugundua shughuli ambayo Hashim alitekeleza kwenye nyumba hiyo
alipaka rangi mpya na kuenda mafichoni.