Visa vya udanganyifu katika mchakato unaoendelea wa mtihani
wa kitaifa kwa watahiniwa wa kidato cha nne vinaendelea kurekodiwa kisa cha
hivi punde kikirekodiwa katika shule ya upili ya Membley eneo la Ruiru, kaunti
ya Kiambu.
Katika siku ya tatu, wanafunzi wawili walipatikana na simu
katika chumba cha mtihani wakati mtihani ulikuwa unaendelea kisa ambacho
kilidhibitishwa na naibu kamishna wa kaunti Julius Too.
Kulingana na afisa wa DCIO eneo la Ruiru Jeremiah Ndubi amesema kuwa simu ya kwanza
ilipatikana wakati wa kuwakagua wanafunzi kabla ya kuingia katika chumba cha
mitihani jambo lililowafanya kufanya ukaguzi zaidi na hatimaye kupata simu
nyingine ikiwa na mwanafunzi wa pili.
Aidha DCIO Jeremiah amehakikisha kuwa mtihani haujaibiwa na
simu zilizopatikana wakati wa mtihani zinakaguliwa kubaini ikiwa zilikuwa
zilikuwa na mitihani au la.
Hata hivyo Jeremiah amesema kuwa kupatikana na simu wakati
wa mtihani ni kinyume na sheria na hatua za kisheria zitachukuliwa dhidi
wahusika waliopatikana kutokakwa baraza kuu la mitihani nchini KNEC.
Licha ya kisa hicho kufanyika , naibu kamishna amesema kuwa
usambazaji wa mitihani katika vituo 18 kwenye kaunti ndogo ya Ruiru inafanyika
vyema.
Tangu mitihani hiyo ya nadharia kung’oa nanga rasmi kote
nchini siku ya Jumatatu, visa kadhaa vya udanganyifu vimerekodiwa katika maeneo
kadhaa.
Mnamo Jumatatu, katika kaunti ya Nairobi na
Kilifi washukiwa wawili walikamatwa kwa kujifanya wanafunzi waliokuwa
wamesajiliwa kama watahiniwa.