Mshauri Mkuu katika Baraza la Washauri wa Kiuchumi katika Ikulu Moses Kuria ameonekana kuunga mkono Kanisa la Katoliki huku likiendelea kupokea ukosoaji kutoka kwa baadhi ya viongozi wa serikali.
Kumekuwa na hisia mseto baada ya Viongozi wa kanisa la katoliki wiki iliyopita kutoa tamko la kuikosoa serikali na kuomba uwajibikaji bora kutoka kwa viongozi.
Katika
taarifa yake siku ya Jumanne, Kuria alisema kuwa yeye ni mshirika dhabiti wa
Kanisa Katoliki na akabainisha kuwa kanisa hilo huwa sahihi kila wakati.
“Sheria zangu mbili kama Mkatoliki ambaye nimepitia mchakato wa Katekisimu kuanzia Ubatizo, Ekaristi Takatifu, Altar Boy hadi kuthibitishwa (Kama Francis) na marehemu Michael Kadinali Otunga wa Kibabii. Kanuni ya 1- Kanisa Katoliki huwa sahihi kila wakati, Kanuni ya 2- Iwapo Kanisa Katoliki limekosea, rejea Kanuni Nambari 1,” Kuria alisema kupitia akaunti yake ya X.
Haya yanajiri siku moja tu baada ya uongozi wa Kanisa la Katoliki katika Dayosisi ya Nairobi kukataa michango ya pesa kutoka kwa wanasiasa.
Siku ya Jumatatu, uongozi wa kanisa la katoliki ulikataa mchango wa pesa uliotolewa na Rais William Ruto na Gavana wa Nairobi Jonson Sakaja wikendi.
Siku ya Jumapili, Rais Ruto alihudhuria ibada katika Kanisa la Katoliki la Soweto jijini Nairobi, akiandamana na Gavana wa Nairobi Sakaja.
Katika barua iliyotiwa saini na Askofu Mkuu Philip Anyoloo, Dayosisi ya Nairobi ilisema Ruto alitoa mchango wa Sh600,000 kwa kwaya ya Kanisa la Katoliki la Soweto na mishonari ya parokia hiyo, huku Gavana Sakaja akichangia Sh200,000.
Rais pia alitoa mchango wa Sh2 milioni za ujenzi wa nyumba ya Baba na aliahidi kulizawadi kanisa hilo basi mnamo Januari mwaka ujao.
Hata hivyo, katika barua ambayo kanisa hilo lilichapisha mtandaoni, Askofu Mkuu Anyolo alisema kuwa Kanisa la Nairobi litadumisha msimamo thabiti kuhusu michango ya wanasiasa, akiangazia hitaji la Kanisa kujilinda dhidi ya kutumiwa kwa malengo ya kisiasa.
"Fedha hizi zitarejeshwa kwa wafadhili husika. Aidha, Sh3 milioni zilizoahidiwa kwa ajili ya ujenzi wa nyumba ya Baba pamoja na michango ya basi la parokia kutoka kwa rais zinakataliwa," inasomeka sehemu ya barua hiyo.
Katika barua hiyo, Anyolo analishauri kanisa kudumisha uadilifu na kukataa michango ambayo inaweza kuhatarisha uhuru wake bila kukusudia.
"Wanasiasa wanashauriwa kuonyesha uongozi wa kimaadili kwa kushughulikia masuala muhimu yaliyoibuliwa na KCCB. Kanisa lazima lisalie kuwa chombo kisichoegemea upande wowote bila ushawishi wa kisiasa ili kutumika kikamilifu kama nafasi ya ukuaji wa kiroho na mwongozo wa jamii,” barua hiyo inasomeka kwa sehemu.
Alhamisi wiki
jana, Baraza la Maaskofu Katoliki Kenya (KCCB) lilidai kuwa kuendelea kutoza
ushuru mpya kwa Wakenya ni njia ya siri ya kuwasilisha tena Mswada wa Fedha
uliokataliwa.
Huku wakikiri kwamba serikali inaweza tu kuongeza mapato yake kupitia kodi, maaskofu walisikitika kwamba raia walikuwa wanatozwa ushuru kupita kiasi.