Maafisa wa polisi kutoka tume ya maadili na kupambana na rushwa nchini EACC wanawachunguza washukiwa wawili wanaodaiwa kuitisha pesa kutoka kwa afisa mkuu mtendaji wa shirika moja la kiserikali kwa njia zisizo halali.
Washukiwa hao, kwa mujibu wa taarifa ya EACC, wanadaiwa kuitisha shilingi milioni mbili kwa mkurugenzi mkuu wa shirika la kiserikali ili kufanikisha kuondolewa kwa kesi iliyowasilishwa mahakamani ya madai ya ufujaji wa pesa za umma katika shirika mkurugenzi huyo analiongoza.
Maafisa wa EACC waliwakamata washukiwa hao Ijumaa wiki jana katika hoteli moja jijini Nairobi baada ya mlalamishi kuwajuza kuhusu tukio ambapo washukiwa walikuwa wanapokezwa shilingi milioni 1.7 kama malipo ya awamu ya kwanza kutoka kwa afisa wa serikali.
Kulingana na polisi, washukiwa hao wanaidaiwa kuwa sehemu ya watu wanaojidai kuwa waendeshaji wa kesi nchini wanaojifanya kuwa raia wa umma na watetezi wa utawala bora ambao huwasilisha malalamisi dhidi ya viongozi wa serikali mahakamani kisha kutaka rushwa kubwa ili kuondoa kesi wanazowakilisha kwenye korti.
Baada ya kukamatwa, wawili hao walihojiwa na maafisa wa EACC
kisha kuachiliwa kwa dhamana ya polisi hatua zaidi zikitarajiwa kuchukuliwa na
tume yamaadili na kupambana na rushwa nchini EACC.