Polisi kutoka Kijabe wameanzisha msako wa kuwatafuta washukiwa watatu wa wizi wa kimabavu waliomwibia dereva mmoja katika daraja kwenye barabara ya Old Kijabe, kaunti ndogo ya Lari katika kaunti ya Kiambu usiku wa kuamkia Alhamisi mwendo wa saa tano.
Washukiwa hao ambao wangali kutambulika, walikuwa wamejihami kwa panga na chombo cha kufungua bomba la maji(pipe wrench) walipotekeleza wizi huo.
Idara ya DCI imearifu kuwa washukiwa hao walifunga barabara katika eneo hilo la daraja kwa kutumia magogo ili kuzuia gari la mwathiriwa dakika chache kabla ya saa tano usiku.
Katika wizi huo, wezi hao walifanikiwa kutoroka na simu aina ya Samsung S22, shilingi elfu sabini na kadi kadhaa za benki. Washukiwa hao wanadaiwa kumshurutisha mwathiriwa kupeana nambari ya siri ya kutoa pesa kwenye simu kisha wakajitumia hela hizo kabla ya kutorokea kichakani.
Aidha mwathiriwa alipata afueni kwa kutorokea katika shule ya Rift Valley Academy baada ya gari lingine lililokuwa linapita katika barabara hiyo kukaribia na washukiwa ambao wanatafutwa sasa kutoroka.
Hata hivyo, baada ya kisa hicho kuripotiwa polisi walifanya msako katika misitu ya karibu na sehemu ya tukio bila mafanikio. Mwathiriwa alisindikizwa hadi nyumbani kwake baada ya kuandikisha ripoti kwenye kituo cha polisi.
Maafisa
wa upelelezi kutoka kaunti ndogo ya Lari wameanzisja msako wa kuwatafuta washukiwa
waliohusika na uvamizi huo wa kimabavu.