Mkuu wa idara ya upelelezi wa makasa ya jinai Mohamed Amin mnamo Ijumaa ameshtumu vikali uvamizi uliofanywa wakati wa ibaada ya mazishi ambapo aliyekuwa naibu wa rais aliyehenguliwa madarakani Rigathi Gachagua alikuwa mmoja wa waombolezaji.
Gachagua siku ya Alhamisi aliilaumu serikali kwa madai ya kufadhili uvamizi dhidi yake wakiwa na nia fiche ya kumwangamiza. Tukio hilo lilitokea katika eneo la Limuru kaunti ya Kiambu wakati naibu rais huyo wa zamani akihudhuria mazishi ya Erastus Nduati, 23, katika kijiji cha Bibirioni.
Hali kadhalika aliyekuwa mbunge wa zamani wa Limuru Peter Mwithi pamoja na mwakilishi wadi wa Bibirioni Christopher Ireri walidaiwa kutekwa nyara katika mazishi hayo kwa kurushwa ndani ya gari aina ya subari zilizokosa nambari za usajili kisha kuwachiliwa eneo la Ruiru.
Mkuu wa idara yaupelelezi wa makosa ya jinai amesema kuwa tukio hilo la Alhamisi bado linachunguzwa na hatua ya kisheria itachukuliwa dhidi ya watu watakaopatikana na hatia ya kuchochea au kupanga vurugu hiyo.
Vile vile Amin aliwahimiza wananchi kuepukana na kusambaza madai ambayo hayajathibitishwa kikamilifu na maafisa wa polisi.
"Kila mmoja anayedai kutekwa nyara anahimizwa kupiga ripoti katika kituo cha polisi ili kuwezesha uchunguzi kufanyika. Pia kama una habari yeyote muhimu inayoweza kutusaidia kufanya uchunguzi na kuwashika wahalifu hao tujuze mapema." Alisema Amin.
Hata hivyo Gachagua aliwanyooshea kidole cha lawama waandani wa rais Ruto ambao hakuwataja majina akiwalaumu kujaribu kugawanya eneo la Mlima Kenya.