Polisi mnamo Alhamisi walifanikiwa kupata risasi 158 pamoja na silaha nyingine za kijeshi kutoka kwa washukiwa wanne waliokamatwa kufuatia msako kwenye kizuizi cha polisi katika kaunti ya Isiolo.
Kwa mujibu wa polisi waliokuwa wakilinda usalama katika barabara ya Marsabit kuelekea Isiolo kwenye eneo la makutano ya barabara ya Hospital, washukiwa hao walikamatwa mwendo wa saa saba na nusu usiku wa kuamkia Alhamisi wakisafirisha silaha hizo kutumia lori aina ya Mitsubishi Fuso.
Katika msako wa polisi kwenye lori hilo, risasi maalum takribani 142 zinazotunika kwa bunduki aina ya AK47, risasi 16 ya milimita 9 inayotumika kwa bunduki ndogo aina ya pistol, seti ya kusafisha bunduki, suruali ndefu na viatu vya kijeshi pamoja na mashati maalum ya kivita ni miongoni mwa bidhaa zilizopatikana katika msako huo.
Washukiwa hao
wanne akiwemo dereva na wanaume watatu wenye umri wa miaka 28, 20 na 18 wanazuiliwa
na polisi pamoja na lori hilo katika kituo cha polisi cha Isiolo huku uchunguzi
wa wakalala mbali mbali wa polisi ukiendelezwa kufuatia upatikanaji wa vifaa
hivyo vya kivita.