Jukwaa la uhuru wa raia CFF limekuwa shirika la hivi punde kuishinikiza kampuni ya mawasiliano ya Safaricom kusitisha vitisho vyake vinavyoelekezwa kwa mshirika mbali mbali ya kutetea haki za kibinadamu na vyombo vya habari.
Kwa ujumbe uliotolewa kwa vyombo vya habari mnamo Jumapili, CFF imeelezea wasiwasi wake kwa Safaricom ikisema kuwa kampuni hiyo inazilenga tume za kutetea haki za kibinadamu ikiwemo tume ya haki za kibinadamu ya Kenya (KHRC), Kundi la Waislamu la haki la binadamu (MUHURI), Kmapuni na Nation Media Group na baadhi ya wanahabari kupitia vitisho vya kisheria na vitendo vya kaudhibu. Kwa mujibu wa CFF, vitisho hivo vinalenga kuvinyamazisha vyombo vya habari na mashirika ya kutetea haki za binadamu dhidi ya kuripoti taarifa za madai ya kampuni hiyo kuhusika katika dhuluma na serikali ya Kenya.
Lalama kutoka kwa mashirika ya kutetea haki za kibinadamu zinajiri baada ya chombo cha habari cha Nation katika taarifa ya ufichuzi iliyotolewa mnamo Ijumaa Novemba 29 kubaini kuwa Safaricom ilihusika katika kutoa taarifa kwa vyombo vya usalama kuhusu walikokuwa baadhi ya washukiwa waliotekwa nyara na wengine kuuliwa maafisa wa polisi wakihusishwa na habari hizo.
Katika uchunguzi wa Nation, ilibainika kuwa Safaricom ilikuwa inatoa data za mahali walikokuwa baadhi ya watu waliopotea visa vya waokupotea vikihusishwa maafisa wa polisi.
CFF imesema kwamba uchunguzi wa Nation ulionyesha jinsi Safaricom huenda ilihitilafiana na mchakato wa utoaji wa haki wakati vyombo vya usalama vilishutumiwa kuhusika na kupotea na mauaji watu.
CFF imeishutumu kampuni ya Safaricom kwa kutumia nguvu zake za kihela na kisiasa kunyanyasa Nation Media Group na wanahabari kwa kutishia kuchukua hatua za kisheria dhidi ya waliohusika na utayarishaji wa ufichuzi huo.
CFF imeikashifu Safaricom kwa kukosa kujibu madai yaliyoelekezwa kwao na badala yake kuelekeza vitisho kwa KHRC na MUHURI mnamo Novemba 18 ikizitaka mashirika hayo kuacha kutoa taarifa kwa umma kuhusu matokeo hayo. Awali, KHRC na MUHURI mnamo Novemba 14, ilikuwa imeiandikia kampuni ya Safaricom barua za kuitaka kujibu madai dhidi yake.
Hata hivyo, jukwaa la uhuru wa raia limeitaka Safaricom
kujibu madai yaliyotelwa dhidi yake na KHRC na MUHURI kupitia barua pamoja na
yale yaliyofichuliwa kwenye uchunguzi wa Nation. Vile vile, CFF imeitaka
Vodafone Group, kampuni inayomiliki Safaricom kuomba radhi kwa kampuni ya
Nation na wanahabari huku ikitangaza kufanya uchunguzi wake wa wazi na huru
kuhusu shughuli za Safaricom.