Seneta wa kaunti ya Homa Bay Moses Otieno Kajwang ameunga mkono mjadala wa ujumuishaji wa pesa za basari kwa kikapu kimoja ili kumfaidi mtoto wa Kenya.
Kwa mujibu wa seneta huyo akizungumza katika kikao cha bunge la seneti mnamo Jumatano, ametofautiana na viongozi wanaopinga ujumuishaji huo akisema kwamba kuweka pesa hizo kwenye kikapu kimoja hakutaondoa CDF wala kupiga vita serikali za kaunti.
“Mjadala huu si wa kuondoa CDF, huu mjadala sio dharau kwa mfuko wa kitaifa wa utekelezaji wa haki za serikali na sio vita kwa serikali za kaunti. Huu mjadala ni kuhusu watoto wa hili taifa.” Alisema Kajwang.
Seneta Kajwang amesema kwamba kujumuishwa kwa hela hizo kutaisadia serikali kuafikia malengo ya elimu yenye ubora kufikia mwaka 2030 kwa wasichana na wavulana wote katika shule za msingi na sekondari kote nchini. Kajwang amekiri kwamba, taifa la Kenya lingali kuafikia malengo hayo licha ya kuwa na ruwaza ya mwaka 2030.
Kwa upande wake seneta wa Nandi Samson Cherargei kwenye mjadala huo, ameunga mkono hoja hiyo akisema kwamba wengi wa maseneta katika bunge la sasa hawangekuwa katika nafasi hiyo ikiwa sio pesa za basari. Ametaka kujumuishwa kwa kwa basari zote ili kuhakikisha kwamba elimu ni ya bure na inaafikiwa na wanafunzi wote.
“Tunahitaji kujumuisha pesa hizo ili kuona kesho yetu.” Alisema seneta Cheragei.
Seneta Cherargei aidha ameitaka tume ya maadili na kupambana na ufisadi EACC kushirikiana na wizara ya elimu na idara ya DCI kuchunguza ufichuzi uliotolewa na runinga moja ya humu nchini kuhusu shilingi bilioni tatu zilizopotea kupitia ufadhili kwa shule ambazo hazipo katika sehemu mbali mbali nchini ikiwemo kaunti ya Baringo.
Vile vile seneta huyo, ameipa changamoto mkaguzi mkuu wa serikali kufanya ukaguzi wa basari zilizotolewa kupitia NGAAF na CDF ambayo ilikuwa kinyume na sheria na kaunti.
“Ofisi ya mkaguzi mkuu lazima ifanye ukaguzi wa kina kwa basari zilizotolewa kupitia NGAAF, CDF yenye ni kinyume cha sheria, serikali za kaunti na ripoti hiyo kuwasilishwa kwenye seneti.” Alisema seneta Cheragei.
Seneta Kajwang na Cherargei wametaka kujumuishwa kwa pesa za
basari ili kumfaidi mtoto wa Kenya kupata elimu ya bure kutoka shule ya msingi
hadi chuo kikuu.