logo

NOW ON AIR

Listen in Live

Tumelipa milioni 500 kwa tuzo za Grammy kuandaliwa Kenya - Rais Ruto

Ruto alisema hayo yanaweza kuthibitishwa na wawakilishi wa Grammys waliokuwepo kwenye mkutano huo.

image
na Samuel Mainajournalist

Yanayojiri10 December 2024 - 12:04

Muhtasari


  • Ruto amefichua kuwa serikali tayari imelipa milioni 500 milioni katika azma ya kuandaa hafla ya tuzo za Grammy mwaka wa 2027.
  • Matamshi ya Rais yalikuja baada ya Dennis Itumbi kusema kwamba rais amewapa ridhaa ya kuomba kuandaa hafla hiyo.


Rais William Ruto amefichua kuwa serikali tayari imelipa Shilingi milioni 500 milioni katika azma yake ya kuandaa hafla ya tuzo za Grammy mwaka wa 2027.

Akizungumza wakati wa mkutano ulioandaliwa Townhall siku ya Jumatatu usiku, Ruto alisema hayo yanaweza kuthibitishwa na wawakilishi wa Grammys waliokuwepo kwenye mkutano huo.

"Pesa za Grammy tayari tumelipa. Tayari tulilipa Sh500 milioni na nina uhakika jamaa kutoka Grammys anaweza kuthibitisha kwamba huo ndio mwelekeo tunakoelekea,” rais alisema.

Matamshi ya Rais yalikuja baada ya Dennis Itumbi, Mkuu wa Miradi Maalum ya Rais na Uchumi wa Ubunifu, kusema kwamba rais amewapa ridhaa ya kuomba kuandaa hafla hiyo.

Itumbi alisisitiza kuwa kuandaa Kongamano la Dunia la Uchumi wa Ubunifu kutasaidia kufungua uwezo wa Kenya katika sekta hiyo.

"Rais tayari ametoa maagizo kwa sisi kuanza kutoa zabuni kwa Mkutano wa Dunia wa Uchumi wa Ubunifu mwaka wa 2027. Ili kuwa nchi ya kwanza ya Kiafrika kuleta sekta ya ulimwengu hapa kwa sababu hiyo itafungua uchumi wote wa ubunifu," alisema.

Rais Ruto aliendelea kusema Mswada wa Ubunifu ambao tayari uko katika Bunge la Kitaifa utafanya mambo kuwa bora zaidi kwa wabunifu nchini.

Rais alisema Mswada utatoa maelekezo thabiti kuhusu masuala ya haki miliki na pia kushughulikia kwa ukamilifu masuala yanayohusiana na uharamia.

“Mswada wa Ubunifu unapitia bungeni ili kuondoa changamoto ambazo umeangazia. Kusasisha sheria ili tuondoe sheria iliyopitwa na wakati na kutoa msingi wa uhakika kuhusu mali miliki na kushughulikia masuala ya uharamia,” Rais alisema.

Rais Ruto amekuwa akitaka sana kufungua uchumi wa kibunifu na kidijitali nchini tangu achukue uongozi wa nchi.

"Mpango wetu unabainisha uchumi wa ubunifu pamoja na utamaduni na urithi kuwa vichochezi vya kuleta mabadiliko na uundaji wa ajira," alisema hapo awali.

Ili kufanikisha hili, Ruto alisema, serikali inatekeleza miswada thabiti ya kisheria ikiwa ni pamoja na Mswada wa Utamaduni ambao tayari uliidhinishwa na baraza la mawaziri.

 "Nyingine kama vile Mfumo wa Ubunifu wa Uchumi, Mswada wa Baraza la Kiswahili la Kitaifa la Kenya, Mswada wa Filamu ya Kenya, Mswada wa Turathi za Kitaifa na Makavazi, zinaandaliwa kwa sasa," alisema.


RADIO JAMBO FREQUENCIES

Kisumu 100.1 | Mombasa 92.3 | Nakuru 96.9 | Eldoret 99.5 | Nyeri 99.3 | Nyahururu 97.3 | Webuye 95.3 | Meru 92.7 | Kitui 104.9 | Kibwezi 104.7 | Voi 105.7 | Malindi 98.1 | Lamu 104.7 | Narok 97.3 | Kapenguria 99.7 | Kisii 89.3 | Garissa 104.3 | Maralal 97.3 | Lodwar 92.7


logo© Radio Jambo 2024. All rights reserved