Takriban watu sita walipoteza maisha yao, na wengine 16 kujeruhiwa vibaya katika ajali mbaya ya barabarani kwenye barabara kuu ya Bomet-Narok mnamo siku ya Jumamosi.
Ajali hiyo, iliyohusisha gari la Nissan matatu na basi la shule ya upili, ilitokea Jumamosi saa kumi na mbili jioni katika daraja la Olonin.
Matatu hiyo ilikuwa ikielekea Narok ilipogongana ana kwa ana na basi lililokuwa likitoka upande mwingine.
Kwa mujibu wa polisi, ajali hiyo ilitokea wakati basi lilipojaribu kuyapita magari yaliyokuwa mbele yake kwa njia isiyo salama.
Kutokana na ajali hiyo, watu watatu waliokuwa kwenye matatu walifariki papo hapo.
Waliojeruhiwa walihamishwa hadi hospitali ya kaunti ndogo ya Ololulung'a ambapo wanawake wawili na msichana mmoja walifariki kutokana na majeraha.
Waliofariki walipelekwa katika Hospitali ya Kaunti ya Narok wakisubiri kutambuliwa na kufanyiwa uchunguzi wa maiti.
Magari hayo mawili yalivutwa hadi katika makao makuu ya polisi ya kaunti ndogo ya Narok Kusini yakisubiri kufanyiwa ukaguzi.
Dereva wa basi hilo, polisi wanasema, alitoroka eneo la tukio na sasa anatafutwa ili kuhojiwa.
Uchunguzi wa awali unaonyesha kuwa aliyapita magari mengine kizembe na kusababisha ajali hiyo.
Ajali hiyo ilitokea saa chache baada ya nyingine kufanyika eneo la Tegero kando ya njia hiyo hiyo na kugharimu maisha ya mwanamke huku wengine watatu wakiponea na majeraha madogo.
Ilihusisha gari la Toyota lililokuwa likielekea Narok na basi la Easy coach kutoka upande mwingine.
Ripoti ya polisi inaeleza kuwa dereva wa Toyota alishindwa kulidhibiti gari hilo lililokuwa likitoka kwenye njia yake na kugongana na basi hilo.
“Ajali hiyo ilihusisha basi lililokuwa likiendeshwa kutoka upande wa Narok kuelekea Bomet likiwa na abiria 34 huku gari lingine aina ya Toyota likiendeshwa kutoka upande tofauti na abiria wanne,” ripoti hiyo ilisema.