Shinikizo linazidi kutolewa na baadhi ya viongozi nchini la kutaka kuachiliwa kwa vijana wanaodaiwa kutekwa nyara na watu wasiojulikana kwa madai ya kumdhalilisha rais katika mitandao ya kijamii haswa kwenye mtandao wa X.
Katika visa vya hivi punde, familia mbili zinaomba kuachiliwa huru kwa wanafamilia wao wanaodaiwa kutekwa nyara baada ya kusambaza picha mtandaoni zinazodaiwa kuwa za kuashiria mauti ya rais. Familia hizo zimetoa wito kwa rais William Ruto kuingilia kati ili vijana hao kuachiliwa huru na kujumuika na familia zao katika msimu huu wa sherehe za krisimasi na mwaka mpya.
Kiongozi wa hivi punde kushtumu utekaji nyara wa vijana hao ni mbunge wa Githunguri Gathoni Wamuchomba ambaye amekashifu utekaji nyara huo kwenye ukurasa wake wa X mchana wa Disemba 24, 2024.
Kulingana na mbunge huyo, amesema kwamba utekaji nyara wa vijana ili kuwanyamazisha ni ishara ya namna nchi imedidimia licha kuwa inatawaliwa na sheria. Wamuchomba amesema kuwa kupotea kwa Billy na Peter ni kati ya visa vingi ambavyo vijana wa kiume wameripotiwa kupotea mikononi mwa watu wasiojulikana.
“Kuwateka nyara vijana ili kuwanyamazisha ni onyesho dogo la jinsi nchi inavyoweza kwenda chini licha ya kutawaliwa na sheria. Kupotea kwa Billy kutoka Embu na Peter kutoka Meru ni wachache tu kati ya vijana wengi ambao wametoweka mikononi mwa watu “wasiojulikana” wanaodaiwa kuwa na nia ya kutesa na kulemaza.” Aliandika Gathoni Wamuchomba kwenye anuani yake ya X.
Wamuchomba ametaka kuachiliwa kwa Kavuli, Peter na Billy wanaodaiwa kutoweka kwa njia tatanishi ikiwemo watu wengine waliotekwa nyara ama wafikishwe mahakamani kwa mujibu wa katiba ya Kenya.
Kiongozi huyo, hata hivyo amesema kwamba kuwanyamazisha kwa
kuwakamata kiholela kutajenga shinikizo kutokana na kutovumilia kwa ukandamizaji
huo amabo umekithiri.
Hayo yakijiri, idara ya polisi bado haijatoa
taarifa kuhusu madai ya kuhusishwa kwa maafisa wake katika utekaji nyara huo.